Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nicaragua sitisha hatua za kuwaandama wapinzani- Wataaalam wa UN

Watu mamia kadhaa wakiandamana katika barabara za Managua, Nicaragua, wakidai haki kwa waathirika wa kamtakamata ya vikosi vya usalama.
OHCHR Regional Office for Centra
Watu mamia kadhaa wakiandamana katika barabara za Managua, Nicaragua, wakidai haki kwa waathirika wa kamtakamata ya vikosi vya usalama.

Nicaragua sitisha hatua za kuwaandama wapinzani- Wataaalam wa UN

Amani na Usalama

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameihimiza serikali ya Nicaragua ikomeshe ukandamizaji kufuatia siku 100 za maandamano ambapo watu  takriban 317 wameuawa ilhali wengine 1,830 wamejeruhiwa.

Maandamano yalikuwa  yanapinga mabadiliko ya mifumo ya hifadhi  ya kijamii,  ingawa hivi karibuni yamepungua kwa idadi na ukubwa wa kiwango chake kufuatia hatua ya serikali ya kuondoa  kwa vizuizi  vya barabarani.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, wataalam hao wamesema ripoti kutoka Nicaragua zinaonyesha kumekuwepo na kile walichokiita “ongezeko la ukandamizaji dhidi ya walengwa fulani na madai ya kuwakamata watu kiholela jambo ambalo linaleta  mazingira ya uoga, na kutojua la kufanya katika jamii fulani na pia katika jamii inayowakilisha mashirika ya kiraia nchini humo.”

Wataalam hao pia wameshangazwa na  hatua ya kuwafungulia mashtaka  ya makosa ya jinai  watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari pamoja na baadhi ya wale wanaopaza sauti dhidi ya serikali, huku wakisema kuwa makundi hayo hubambikiziwa makosa kama vile ya ugaidi. 

 

Waandamanaji wakiwa Managua wakiandamana kutaka kukomeshwa kwa ukatili Nicaragua
Artículo 66
Waandamanaji wakiwa Managua wakiandamana kutaka kukomeshwa kwa ukatili Nicaragua

 

Halikadhalika wamesema mwezi Aprili mwaka huu, vikosi vya usalama vikisaidiwa na makundi ya wanamgambo wa chama tawala vilisambaratisha waandamanaji vikitumia nguvu kupindukia.

Mbali na hali hiyo , wataalam  wa  Umoja wa Mataifa wanasema wapinzani wa serikali kama vile waalimu, madaktari, wanafunzi, viongozi wa kijamii, waandishi habari wa kujitegemea pamoja na wajumbe wa  kanisa katoliki bado wanatishiwa na kupokonywa uhuru wao huku wakilundikwa korokoroni, na maafisa wa afya wanaowapatia huduma wale waliojeruhiwa wamefukuzwa kazini bila sababu maalum.

 

Waandamanaji mjini Managua wakidai kukomeshwa kwa ghasia nchini Nicaragua
Artículo 66
Waandamanaji mjini Managua wakidai kukomeshwa kwa ghasia nchini Nicaragua

 

Kwa mantiki hiyo wameisihi Nicaragua iepuke kujihusisha na vitendo vya kuharamaisha watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wengine ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya sheria za usalama wa taifa na zile za kukabiliana na ugaidi.