Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 25 wameuawa Nicaragua wakati wa maandamano: UN

Picha: UM/Video capture
Bi. Liz Throssell, msemaji wa Ofisi ya UNHCR.

Watu 25 wameuawa Nicaragua wakati wa maandamano: UN

Amani na Usalama

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema imepokea taarifa za kuaminika kwamba takriban watu 25 wameuawa nchini Nicaragua wakati wa maandamno ya nchi nzima dhidi ya mipango ya kufanyia mabadiliko mfumo wa hifadhi ya jamii.

Ofisi hiyo inasema inatiwa hofu kwamba vifo hivyo huenda ikawa ni mauaji ya kinyume cha sheria.

Imetoa wito kwa serikali ya Nicaragua kuhakikisha kunafanyika haraka uchunguzi huru, wa kina na ulio wazi kufuatia vifo hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva hii leo msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Liz Throssell amesema ni muhimu madai yote ya polisi na vikosi vingine vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi yakachunguzwa ipasavyo na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.

Pia ofisi ya haki za binadamu imesema inatiwa mashaka na taarifa za idadi kubwa ya watu kujeruhiwa au kushikiliwa mahabusu katika siku kadhaa zilizopita, hivyo imetaka kufanyika uchunguzi wa vitendo vyote vya ghasia, ikiwemo uporaji unaodaiwa kufanywa na waandamanaji.

Ingawa Rais wa Nicaragua Daniel Ortega ametangaza kusitisha mipango hiyo ya mabadiliko lakini bado maandamano mengine huenda yakafanyika.

Umoja wa Mataifa umerejerea wito wake kwa serikali hiyo kuheshimu wajibu wake chini ya sheria za kimataifa na kuhakikisha watu wake wakiwemo watetezi wa haki za binadamu wanaweza kutumia haki yao ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani na pia wametoa wito wa kukomesha mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.