Uhakika wa chakula ni mtihani mkubwa kwa watu wa jamii za asili: FAO
Uhakika wa chakula umeelezwa kuwa ni changamoto kubwa kwa watu wa jamii za asili hususan wanawake ambao ndio walezi wa familia na jamii.
Hayo ni kwa mujibu wa Yon Fernandez de Larrinoa ambaye ni kiongozi wa timu ya watu wa jamii za asili katika shirika la chakula na kilimo FAO.
Ameongeza kuwa kuna jumla ya wanawake wa jamii za asili milioni 185 kote duniani ambao ni wavuvi, wawindaji, waokota matunda na watetezi wa ardhi na rasilimali zao, lakini licha ya mchango wao mkubwa wa kiuchumi na kijamii mara nyingi wanatengwa na kutohusishwa katika mchakato wa kufanya maamuzi yanayowahusu.
Pia amesisitiza kuwa kuheshimu hali, na mchango wa watu wa jamii za asili ni muhimu kwani imekuwa kawaida kwa kazi zao kutothaminiwa, hawalipwi ujira unaostahili na wanadharauriwa kila wakati.