Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watakaohusishwa na unyanyasaji wa kingono hawana kazi UNHCR

Baadhi ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan kusini wakizungumza na viongozi wa Umoja wa Mataifa
UN Photo/Isaac Billy
Baadhi ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan kusini wakizungumza na viongozi wa Umoja wa Mataifa

Watakaohusishwa na unyanyasaji wa kingono hawana kazi UNHCR

Haki za binadamu

Pamoja na jitihada za kupiga vita unyanyasaji wa kingono na ukatili, dhidi ya waathirika wa kivita katika maeneo ya migogoro  duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR sasa limegeuzia harakati hizo kwa wafanyakazi wake ili  kutokomeza vitendo hivyo viovu.

Akizungumza na vyombo vya habari mapema mwezi huu, Bi Diane Goodman ambaye ni mratibu mkuu wa UNHCR kuhusu unyanyasaji wa kijinsia amesema, pamoja na kwamba shirika hilo limejitolea kuokoa maisha ya mamilioni ya waathirika mbalimbali duniani  haliwezi kuvumilia tuhuma na pia vitendo hivyo kwa wafanyakazi wake.

Sauti ya Diane Goodman

 "Vitendo hivyo vinakiuka misingi ya UNHCR  na ni kinyume na  maadili yetu. Vile vile ni muhimu kufahamu kwamba kuna zaidi ya wafanyakazi 15,000 wa UNHCR ambao wanafanya kazi ya kujitolea kuwasaidia na kuwahudumia wakimbzi katika mazingira magumu sana. Na wale ambao wamehusishwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia  kwa wakimbizi hawana nafasi katika UNHCR."


Aidha Bi Diane amesema, UNHCR inaendelea kufanya kazi kwa utaratibu mahususi katika kutambua na kupunguza vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na hatari ya unyanyasaji wa kijinsia, pia kutokomeza  ukatili wa aina yoyote katika  kuzingatia maadili na mitazamo ambayo inaendana maadili ya shirika .

Hivi karibuni kumekuwepo na tuhuma zikiwahusihsa wafanyakazi wa UNHCR wa ngazi mbalimbali na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ambapo shirika hilo limeanzisha uchunguzi ili kubaini wahusika na  baadaye kuwachukulia hatua za kisheria.