Cambodia achia huru mliowakamata wakati wa uchaguzi- OHCHR

17 Agosti 2018

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, imesema ina wasiwasi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Cambodia kufuatia ripoti ya kwamba uchaguzi mkuu  ulifanyika mwishoni mwa mwezi uliopita bila ushiriki wa chama kikuu cha  upinzani cha CNRP kilichofutwa.

Ravina  Shamdasani ambaye ni msemaji wa OHCHR mjini Geneva, Uswisi amesema  wasiwasi wao unazingatia ukweli kwamba kwa kufutwa kwa chama hicho, idadi kubwa ya wananchi walinyimwa fursa yao ya kuchagua wawakilishi wao, na hivyo kutia hofu juu ya haki ya ushiriki wao kwenye siasa.

Inaripotiwa kuwa watu walitishiwa au walilipwa ili wapige kura, na mashirika ya kiraia yalikumbwa na manyanyaso na vizuizi kuelekea uchaguzi.

Bi. Shamdasani ameongeza “wavuti mashuhuri zilizuiwa siku ya uchaguzi na vikwazo pia viliwekwa kuhusu uhuru wa kujieleza kwa wapiga kura na wapinzani wa kisiasa waliotoa wito wa kususia uchaguzi huku wengine wakikamatwa na kuwekwa ndani wakitishiwa kukabiliwa na hatua za kisheria.”

Msemaji huyo ameongeza kuwa kwa kuwa hivi sasa matokeo ya uchaguzi yameshatangazwa, “tunahimiza serikali iwaachilie huru wapinzani wa kisiasa, waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu, na wananchi wa kawaida, ambao wamefungwa kizuizini kwa kutumia haki zao za kibinadamu, hasa haki ya uhuru wa kujieleza."

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter