Myanmar achia huru waandishi wa habari wa Reuters -UN

Mjumbe maalum wa haki za binadamu kuhusu Myanmar Yanghee Lee
Picha/Jean-Marc Ferré
Mjumbe maalum wa haki za binadamu kuhusu Myanmar Yanghee Lee

Myanmar achia huru waandishi wa habari wa Reuters -UN

Haki za binadamu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wana wasiwasi baada ya  mahakama nchini Myanmar kuwafungulia rasmi mashtaka waandishi wa habari wawili wa shirika la habari la Reuters.

Wanahabari hao walishtakiwa Jumatatu chini ya sheria ya mwaka 1923 inayohusu siri maalum za serikali na wanakabiliwa na shtaka la kukutwa na nyaraka za siri za serikali, kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka 14 jela.
 
Waandishi hao wa habari Wa Lone na Kyaw Soe Oo walikamatwa baada ya kuandika habari ya uchunguzi kuhusu mauaji yaliyofanyika katika kijiji cha Inn Din, jimbo la Rakhine.
 
Wataalam hao,  Yanghee Lee, ambaye anahusika na hali ya haki za kibinadamu nchini Myanmar na David Kaye, anayehusika na kuendeleza  na kulinda  uhuru na haki za kujieleza, wakizungumza huko mjini Geneva Uswisi, wamekariri wito wao wa kuwataka waandishi habari  hao kuachiliwa huru mara moja na kufuta mashataka dhidi yao.
 
“Mashtaka hayo yanafanya uchunguzi wa kina wa habari hususan kuripoti kuhusu  ukiukwaji wa haki za binadamu katika jimbo la Rakhine kuwa kosa la jinai,” wamesema.
 
Wataalam maalum wamekuwa wakipigania  kuachiwa huru kwa waandishi habari hao baada ya kukamtwa kwao na kuiomba serikali ya Myanmar kufuta mashtaka dhidi yao.
 
Pia wameomba kuangaliwa upya kwa  sheria kuhusu hati maalum za siri ili  iendane na sheria za kimataifa huku wakisema wataendelea kuwasiliana  na serikali ya Myanmar kuhusu kesi hiyo.