Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali na wanasiasa Comoro heshimuni haki za binadamu- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kulia) akihutubia kikao cha amani na usalama cha
UNOAU/Edda Zekarias
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kulia) akihutubia kikao cha amani na usalama cha

Serikali na wanasiasa Comoro heshimuni haki za binadamu- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea hofu yake juu ya kuendelea kwa vizuizi vya uhuru na haki za kidemokrasia nchini Comoro wakati huu ambapo nchi hiyo inaelekea katika kura ya maoni kuhusu katiba kesho Jumatatu.

Katika taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na naibu msemaji wake, Bwana Guterres amesihi, “serikali, vyama vya siasa na wadau wote husika kufanya kila jitihada kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu.”
 
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, upigaji kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya  kikatiba ni pendekezo la Rais Azali Assoumani, ambaye aliingia madarakani miaka miwili iliyopita na  ambaye amekuwa akishutumiwa na wapinzani wa kisiasa kwamba kura hiyo itakayopigwa kesho ni jitihada za kuongeza muhula mwingine katika uongozi wake tofauti na katiba ya sasa ambayo inamruhusu rais kugombea kwa muhula mmoja tu.
 
Halikadhalika, kwa mujibu wa katiba ya sasa, urais wa Comoro unazunguka kila baada ya miaka mitano baina ya visiwa vikuu vitatu vya Comoro ambavyo ni Ngazija ambayo ni Comoro Kuu, Moheli na Anzouan.
 
Mzunguko huo ni njia ya kuweka  mizania ya utawala baada ya miaka mingi ya vurugu za kivita.
 
Ripoti zinasema kuwa makamu wa rais wote  watatu kutoka visiwa vikuu wanamuunga mkono rais katika mchakato wa kupitisha kura ya maoni  na kuimarisha mamlaka yake zaidi.
 
Mnamo mwezi Juni mwaka huu,  mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika AU, ambayo imesaidia kuimarisha mchakato wa uchaguzi katika visiwa vya  Comoros, alitoa wito kuhusu "makubaliano mapana katika kufikia mwafaka" juu ya mabadiliko ya taasisi katika  visiwa hiyo.