Walinda amani wa UN washambuliwa nchini Mali, wawili wapoteza maisha.

27 Oktoba 2018

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, umeripoti kuwa  hii leo walinda amani wawili wa umoja huo kutoka Burkina Faso wameuawa na wengine 11 wamejeruhiwa kutokana na shambulizi la kupangwa lililotekelezwa alfajiri ya leo katika kambi ya MINUSMA iliyoko Ber kaskazini mwa nchi hiyo. 

Taarifa kutoka MINUSMA imesema kuwa walinda amani walioko katika eneo la Ber karibu na Timbuktu wamekabiliana na shambulio zito lililotekelezwa na wapiganaji waliokuwa na silaha nzito za kivita.

Walinda amani hao awali waliwafurusha washambuliaji ambao hawakufahamika na saa chache baadaye katika eneo la Mopti, walinda amani wakashambuliwa tena safari hii kwa kutumia vilipuzi vilivyounda na washambuliaji.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ndiye mkuu wa MINUSMA, Maamat Saleh Annadif amaeeleza kusikitishwa na shambulizi hili lililotekelezwa na aliowaita “maadui wa amani.”

“Ninalaani vikali shambulizi hili la kikatili ambalo halitasitisha mpango wetu wa kuisaidia Mali katika njia yake ya kuelekea kwenye amani. Watekelezaji wa makosa haya ni lazima washitakiwe na wawajibike kwa makosa yao”,amesema Maamat.

Mkuu huyo wa MINUSMA ametuma salamu zake za rambirambi kwa wanafamilia wa walinda amani waliopoteza maisha na amewatakia wote waliojeruhiwa kupona haraka. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake amelaani shambulio hilo dhidi ya kambi ya MINUSMA huko Ber, pamoja na shambulio lingine kwenye eneo la Konna ambalo limesababisha walinda amani wanne kutoka Togo kujeruhiwa.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia na serikali ya Burkina Faso huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi kutoka Burkina Faso na Togo.

Bwana Guterres amesekumbusha kuwa shambulio lolote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa linaweza kuwa uhalifu wa kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa na ametaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Kuibuka kwa makundi ya wapiganaji yenye silaha yanayopambana na vikosi vya serikali na washirika wake katikati na kaskazini mwa Mali kufuatia kushindwa kwa mapinduzi miaka sita iliyopita, kumeifanya MINUSMA kuwa ujumbe hatari wa kuhudumu nao katika Umoja wa Mataifa.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter