Heko Mali kwa kampeni tulivu, kesho chagueni rais kwa amani- UN

28 Julai 2018

Kuelekea uchaguzi wa rais nchini  Mali hapo kesho Agosti 29, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutereres amesema anatiwa moyo na jinsi ambavyo kumekuwepo na amani wakati wa kampeni licha ya changamoto za usalama kwenye maeneo ya kaskazini na kati mwa taifa hilo la Mali.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres amesema ni kwa mantiki hiyo anafuatilia kwa ukaribu uchaguzi  huo huku akitoa wito kwa serikali ya Mali na wananchi wake kuzingatia usalama wakati wanaenda kumchagua kiongozi wao.
 
Ni muhimu kudumisha amani, na kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Jumapili unakumbukwa kama adhimisho muhimu la demokrasia,” amesema Katibu Mkuu.
 
Amewataka wapiga kura katika taifa hilo lenye takribani  watu milioni 18, wajitokeze kwa wingi kumchagua kiongozi wanaompenda katika hatua hiyo muhimu ya kidemokrasia.

Aidha Bwana Guterres amewahimiza wanasiasa wote "kujitolea kufanya mchakato wa uchaguzi huu kuwa   wa amani,  huru na uwazi na kutatua migogoro na tofauti zao  zinazoweza kujitokeza kupitia taasisi husika kwa mujibu wa sheria."

Katibu Mkuu amesisitiza  kuwa amani na upatanisho kwa wananchi wote wa Mali ni jambo mtambuka bila kujali matokeo ya uchaguzi huku akisisitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa kwa jumla, kuendeleza mchakato wa uchaguzi huo.

Jumla ya wagombea 24 wanawania kiti cha urais nchini Mali huku Rais Ibrahim Boubacar Keita na mgombea Soumaila Cisse wakionekana kuwa wagombea walio na ushawishi mkubwa.

Uchaguzi huu unafanyika miaka sita baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani Rais Amadou Toumani Toure na kutumbukiza Mali kwenye mzozo ulioibua waasi wanaotaka kujitenga kudhibiti theluthi mbili ya eneo la Mali.

Rais Keita aliingia madarakani baada ya uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 2013. ambapo serikali yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiusalama wakati ikijaribu kurejesha hali ya amani.

Hata hivyo kwa msaada ya jamii ya kimataifa, ilifanikiwa kupambana na jaribio la kutaka kupindua serikali madarakani ambapo mji wa kale wa Timbuktu ulishambuliwa na waasi na kusababisha vifo vya askari wengi walinda wa amani wa Umoja wa Mataifa .

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter