Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya purukushani, uchaguzi wafanyika kwa amani Mali

Walinda amani wa MINUSMA washika doria nchini Mali wakati wa upigaji kura.
MINUSMA/Harandane Dicko
Walinda amani wa MINUSMA washika doria nchini Mali wakati wa upigaji kura.

Licha ya purukushani, uchaguzi wafanyika kwa amani Mali

Amani na Usalama

Nchini Mali uchaguzi wa rais umefanyika kwa amani licha ya kuripotiwa kwa visa vya hapa na pale vilivyokwamisha upigaji kura kufanyika katika baadhi ya vituo.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa  habari mjini New York, Marekani hii leo kuwa kwa mujibu wa serikali ya Mali, mivutano iliyotokea imesababisha kura kutopigwa katika vituo 644 kati ya vituo 4,632 kwenye maeneo ya kati na kaskazini mwa Mali.

Miongoni mwa visa hivyo ni shambulio la makombora 10 yaliyoelekezwa kwenye kambi ya Aguelhok ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA.

Kambi hiyo iko jimbo la Kidal kaskazini mwa Mali, ambapo shambulio hilo licha ya kutosababisha madhara ya vifaa au majeruhi, lilisababisha kusitishwa kwa upigaji wa kura.

 

Mama mmoja apiga kura katika kituo kilichoko Bamako katika uchaguzi wa urais 29 Julai 2018
MINUSMA/Marco Dormino.
Mama mmoja apiga kura katika kituo kilichoko Bamako katika uchaguzi wa urais 29 Julai 2018

 

Hata hivyo Bwana Haq amesema wanatumai kuwa kazi ya kuhesabu kura itafanyika kwa uwazi ili matokeo yaweze kukubaliwa na pande zote.

Matokeo ya kwanza ya uchaguzi  yanatarajiwa ndani ya saa 48 ambapo matokeo rasmi yanatakiwa yawe yametangazwa ifikapo Ijumaa.

Hata hivyo yaelezwa kuwa iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, awamu ya pili ya uchaguzi wa rais itafanyika tarehe 12 mwezi ujao wa Agosti.