Zimbabwe chonde chonde zingatieni ahadi ya amani- Guterres

2 Agosti 2018

Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kutokana na matukio ya ghasia yaliyoibuka nchini Zimbambwe baada ya uchaguzi wa rais na kusababisha vifo vya raia.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa watu watatu waliuawa kwenye mji mkuu Harare wakati wa vuta nikuvute iliyofuatia uchaguzi huo uliofanyika tarehe 30 mwezi uliopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia Naibu msemaji wake ametaka pande husika Zimbambwe zirejelee ahadi zao walizotoa katika tamko la ahadi ya uchaguzi na kanuni za mwenendo ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

Ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wananchi wa Zimbabwe wajizuie na kukataa aina yoyote ya ghasia wakati huu ambapo wanasubiri tangazo la matokeo rasmi ya uchaguzi huo.

Bwana Guterres pia ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wagombea kwenye nafasi hiyo ya urais wasake suluhu zozote za tofauti zitakazojitokeza kwa njia ya amani, mashauriano na sheria.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, uchaguzi huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya demokrasia Zimbabwe.

Amesema anatambua mwenendo wa amani na demokrasia ambavyo viliripotiwa na waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa siku ya kupiga kura.

Amepongeza azma ya wananchi wa Zimbabwe ya kuimarisha demokrasia na kujikita tena kwenye maendeleo ya nchi yao.

TAGS: Zimbabwe, Antonio Guterres, Uchaguzi

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter