Licha ya hatari na uhaba wa fedha, ulinzi wa amani bado ni nyenzo muhimu:Lacroix

30 Julai 2018

Licha ya kupunguzwa kwa bajeti na kuongezeka kwa majeruhi na vifo miongoni mwa walinda amani, bado ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa unabakia kuwa nyenzo muhimu katika kuchagiza amani na utulivu duniani, amesema mkuu wa operesheni za ulinzi wa aman iza Umoja wa Mataifa. 

Akizungumza na UN News, Jean-Pierre Lacroix ameelezea jinsi gani mkakati wa kuchukua hatua kwa ajili ya ulinzi wa amani uliozinduliwa hivi karibuni unavyonuia kuchagiza uungaji mkono kutoka nchi wanachama katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye operesheni hizo.

Pia amesisitiza haja ya kuwaandaa walinda amani kwa mazingira ya hatari yanayoongezeka"Ni lazima tuimarishe mafunzo kwa askari wetu polisi na wanajeshi, ni lazima tuhakikishe wana vifaa sahihi, lazima tuhakikishe kwamba wanaongozwa vizuri na lazima tuhakikishe kuna uwajibikaji katika kila ngazi ya uongozi. Lakini pia nadhani ni muhimu kuhakikisha majukumu yetu yanajikita katika vitu muhimu." 

Na kwa upande wa ukata unaokabili operesheni hizo  Jean-Pierre Lacroix amesema

"Nadhani pia ni muhimu kuendelea kila wakati kubana matumizi, hiki ni kitu ambacho nchi wanachama wanatutarajia kukifanya, nafikiri ni kitu kizuri na pia kinatufanya tuwajibike zaidi, lakini ulinzi wa amani una gharama na hivyo hatuwezi kupindukia katika kupunguza rasilimali zetu , tunahitaji rasilimali za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yetu, hususan tunapofanya juhudi zote hizi kukabiliana na hali ya usalama tunayokabiliana nayo sasa."

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter