Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvuvi ndio uhai wetu na maisha yetu , lakini sasa ni mtihani-Wanawake Chad

Mvuvi Falmata Mboh Ali (kulia) akiwa na mwenzake kwenye ziwa Chad wakisaka samaki ambao idadi yao imepungua kutokana na kusinyaa kwa ukubwa awa ziwa hilo.
UN News/Dan Dickinson
Mvuvi Falmata Mboh Ali (kulia) akiwa na mwenzake kwenye ziwa Chad wakisaka samaki ambao idadi yao imepungua kutokana na kusinyaa kwa ukubwa awa ziwa hilo.

Uvuvi ndio uhai wetu na maisha yetu , lakini sasa ni mtihani-Wanawake Chad

Tabianchi na mazingira

Navua samaki kwa miaka ishirini,  na sasa inazidi kuwa vigumu kupata samaki, ni kauli ya mvuvi mwanamke huko nchini Chad ambaye mabadiliko ya tabianchi na matumizi holela ya maji kwenye bonde la Ziwa Chad yameleta shida kwenye familia yake

Changamoto za mabadiliko ya tabianchi na udhibiti mbaya wa maji , vinawaweka roho juu wanawake wavuvi nchini Chad ambao mlo na maisha yao ya kila siku hutegemea uvuvi, sasa samaki wameanza kuadimika na kuwaongezea mtihani wa kiuchumi na kijamii. Flora Nducha na taarifa kamili

Navua samaki kwa miaka ishirini,  na sasa inazidi kuwa vigumu kupata samaki

Huyo ni Bi Falmata Mboh mwenye miaka 50, amedamka asubuhi na mapema kijijini Bol, nje kidogo ya mji mkuu wa Chad, N’djamena, akiwa ndani ya ngalawa yake kuvua samaki ziwa Chad.

Hadi sasa amepata kama samaki 50 baada ya kurusha nyavu kwa takriban saa tano japo si haba lakini hawakidhi mahitaji ya familia yake ya watoto 11

“Naweza kuuza samaki hawa na kutumia fedha kununua nafaka kulisha familia yangu, lakini nafaka hiyo haifiki mbali.”

Uvuvi ndio mhimili wa jamii hizi za bonde la ziwa Chad ukisaidia takribani watu milioni 30 wanaoishi kandoni mwa ziwa hilo lakini pia Cameroon, Nigeria, na Niger.

Idadi ya wanawake kwenye bonde la Ziwa Chad huko Afrika Magharibi wanaojihusisha na uvuvi inazidi kuongezeka na sasa wanavua na hata kupaa ili waweze kuuza na hatimaye kupata kipato.
UN News/Dan Dickinson
Idadi ya wanawake kwenye bonde la Ziwa Chad huko Afrika Magharibi wanaojihusisha na uvuvi inazidi kuongezeka na sasa wanavua na hata kupaa ili waweze kuuza na hatimaye kupata kipato.

Lakini sasa ziwa hilo limesinyaa moja ya kumi ya ukubwa wake kutokana na mabadikliko ya tabia nchi na udhibiti mbovu wa maji maji, samaki wanazidi kuadimika na kuwafanya wavuvi kwenda mbali kusaka.

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP limeingilia kati kuokoa jahazi

“Tumesaidiwa na mradi ambao unagawa nyavu mpya, hivyo idadi ninayopata inaongezeka, sasa nina matumaini kwamba maisha ya familia yangu yatabadilika.”

Hatua zinazochukuliwa na wanawake hawa wavuvi ni ndogo lakini ni za muhimu sana kwa mujibu wa mkuu wa msafara Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed kwa hiyo…

 (Sauti ya Amina J. Mohammed)

“Tunaona uvuvi hapa ziwa Chad, lakini tunapaswa kushuhudia mchango huu kwenye mfumo mzima wa thamani, ili pindi wanapovua wanaweza kuchaka na kupeleka sokoni, wapate bei nzuri. Tuweze kutumia teknolojia bora ya kurahisisha kiwango kikubwa cha uzalishaji na mauzo kwenye sekta hii ya uvuvi ambayo wameamua kushiriki.”

Kwa sasa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa wanasaidia juhudi za nchi zilizoko bonde la Ziwa Chad ili kufufua matumaini mapya ya ukanda huo.