Ama  hakika wanawake Somalia wamejizatiti kusongesha amani- UN/AU

23 Oktoba 2019

Ukiwa ziarani kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishi hii leo, ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU, umekaribisha mafanikio yaliyopatikana kwenye taifa hilo la pembe ya Afrika katika ushiriki wa wanawake kwenye masuala ya amani, usalama na maendeleo huku ukitoa wito wa kutaka mafanikio zaidi. 

Kiongozi wa ujumbe huo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed akisema kuwa, “baada ya miongo kadhaa ya mizozo katikati ya mzozo unaondelea nchini Somalia, taifa hilo limepata maendeleo makubwa katika mwelekeo wa amani an utulivu.”

Bi. Mohammed amesema wakati wa ziara yao fupi nchini humo, wamesikia kutoka kwa viongozi wa serikali na wale wa mashirika ya kiraia jinsi ambavyo ushiriki wa wanawake wa taifa hilo katika harakati za amani umesaidia taifa hilo kuelekea katika mustakabali jumuishi na wenye amani.

“Huu ni mustakabali unaofaa wananchi wa Somalia na ambao Umoja wa Mataifana AU wanaunga mkono kwa dhati,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo amesema bado kuna mengi ya kufanya hususan katika kufikia usawa wa jinsia, ikiwemo wanawake kushiriki kwa ukamilifu kwenye suala la mtu mmoja kura moja wakati wa uchaguzi mkuu wa serikali kuu mwakani.

Amesema, “tunakaribisha mafanikio ya hivi karibuni, hususan kwenye maeneo ya haki za binadamu, masuala ya uraia na ushiriki wa siasa, upataji wa haki na huduma za msingi.”

Wakati wa ziara hiyo Bi. Mohammed aliungana na Mjumbe Maalum wa AU katika masuala ya wanawake, amani na usalama, Bi. Bineta Diop na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa pembe ya Afrika Parfait Onanga-Anyanga.

Lengo la ziara hiyo ya siku moja lilikuwa kuelezea azma ya Umoja wa Mataifa na AU katika kusaidia watu wa Somalia kwenye kusaka kwao amani, utulivu na kufanikisha uchaguzi huru, haki na halali.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J.Mohammed kusosho akizungumza na waziri wa wanawake na haki za binadamu wa Somalia , Deeqa Yasin mjini Moghadishu
UNSOM/John Arigi
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J.Mohammed kusosho akizungumza na waziri wa wanawake na haki za binadamu wa Somalia , Deeqa Yasin mjini Moghadishu

 

Ujumbe huo wa AU na Umoja wa Mataifa ulikuwa na kikao na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifaya Uchaguzi Somalia, Bi. Halima Ismail Ibrahim pamoja na kundi la viongozi wanawake kutoka mashirika ya kiraia ambapo walijadili kwa kina suala la mtu mmoaj kura moja na jinsi ya kukabiliana na misimamo mikali.

“Fursa ya kusikiliza sauti tofauti kuhusu nafasi ya wanawake wa Somalia wenye dhima tofauti kwenye  jamii zao, kumeonyesha ni jinsi gani walivyohamasika na wanavyoshiriki na wanavyojizatiti kuhakikisha kuwa dhima ya wanawake na usawa wa jinsia vinajumuishwa katika maeneo yote ya kijamii,” amesema Bi. Mohammed.

Naye Bi. Diop akiwasilisha ujumbe wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Moussa Faki amesema, “naamini kwa dhati juu ya dhima muhimu ya wanawake katika operesheni za amani. Nawavulia kofia kwa kujitoa kwao na azma yao ya dhati kwenye amani na utulivu kwa misingi ya majukumu ya AMISOM.”

 Bi. Diop ametoa kauli hiyo kwa kuzingatia kuwa pia alikutana na walinda amani wanawake wanaohudumu kupitia ujumbe wa Muungano wa Afrika, Somalia, AMISOM.

Ziara hiyo Somalia, ni sehemu ya ziara ya siku sita ya ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa na AU kwenye pembe ya Afrika.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter