Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani Chad, Naibu Katibu Mkuu apazia nafasi ya wanawake

Wanawake nchini Chad wakichuuza mboga kwenye soko lisilo rasmi angalau kupata kipato cha kujikidhi maisha yao kwa kuwa mashambulizi ya Boko Haram na ukame vinakwamisha maisha  yao.
OCHA/Naomi Frerotte
Wanawake nchini Chad wakichuuza mboga kwenye soko lisilo rasmi angalau kupata kipato cha kujikidhi maisha yao kwa kuwa mashambulizi ya Boko Haram na ukame vinakwamisha maisha yao.

Ziarani Chad, Naibu Katibu Mkuu apazia nafasi ya wanawake

Amani na Usalama

Naibu Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed yuko ziarani nchini Chad ambako amesisitiza jukumu muhimu la wanawake wa nchi hiyo katika kukabiliana na changamoto za Boko Haram na uchochezi wa ukatili.

Bi. Mohammed amesema hayo leo katika mikutano tofauti huko Bol, kaskazini mwa mji mkuu wa Chad, N’Djamena ambako amekutana na jamii mbalimbali zinazojaribu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Amekutana pia na vikundi vya kidini, vijana na wanawake.

“Cha msingi ambalo pia ni jambo la kawaida kwenye eneo hilo ni kutumikishwa kwa wanawake na wasichana hivyo ndio sababu usawa wa kijinsia lazima uwe msingi wa juhudi za kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji huo,” amesema Naibu Katibu Mkuu.

Bi. Mohammed alikutana na msichana aliyelazimishwa na Boko Haram kuwa mshambulizi wa kujitoa mhanga ambaye alipoteza miguu yote miwili wakati bomu lilipolipuka.

Naibu Katibu Mkuu amesema mwanamke huyo, ambaye sasa anafanya kazi kuhamasisha wanawake na wasichana wengine dhidi ya misimamo mikali na ukatili uliokithiri amegeuka kutoka mhanga hadi manusura.

Kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na usimamizi duni wa ardhi na watu mashinani amesema watu wote wanachangia katika ukataji miti Ziwa Chad, eneo ambalo ni makazi ya watu milioni 50.

Mwanamke akinunua tende kwenye soko moja lililoko mji wa Bol, nje kidogo ya mji mkuu wa Chad, N'djamena.
OCHA/Pierre Peron
Mwanamke akinunua tende kwenye soko moja lililoko mji wa Bol, nje kidogo ya mji mkuu wa Chad, N'djamena.

Ametaka usimamizi bora kwa kuwa ziwa Chad ni chanzo cha kipato kwa watu milioni 2, na wengine milioni 13 wanategemea bonde la ziwa hilo huku akisema.

“Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni nyenzo muhimu kwa fursa zao za uongozi na nafas iza kufanya maamuzi, nina wachagiza wanawake kushiriki katika michakato yote ya kisiasa, amani, usalama na maendeleo ambayo itaendeleza jamii zao.”

Kwa upande wake mjumbe maalum wa Muungano wa Afrika kuhusu wanawake, amani na usalama Bineta Diop ambaye amezungumzia umuhimu wa kile alichoshuhudia na mchango wake katika kuhifadhi na kutunza ziwa Chad na bonde lake.

“Sasa hivi wanawake wanashika umiliki na usukani wa uongozi na hiki ndicho tunachokibaini Afrika katika maendeleo. Lazima tuwafanye wanawake wawe kitovu  kwa sababu wanajua, wanaelewa na wanajua endapo ziwa litatoweka nao watatoweka hivyo wataliangalia vizuri, hivyo tuko hapa kuunga mkono mradi huu wa wanawake ambao ni uti wa mgongo wa Kijiji hiki katika jamii hii.”

Viongozi wengine waliombatana na Naibu Katibu Mkuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Wallström.