Kuna nuru Sudan Kusini licha ya changamoto- Bi. Mohammed

4 Julai 2018

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Sudan Kusini hii leo akisema kuna dalili za ustawi nchini humo licha ya changamoto zilizopo.

Bi. Mohammed amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, mazungumzo ambayo yameripotiwa kupitia mtandao wa Twitter wa radio Miraya iliyo chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Amesema jambo muhimu ni kuendelea kuwa na matumaini ingawa kuna changamoto ikiwemo ukosefu wa usalama, ukiukwaji wa haki za binadamu na changamoto pia za kibinadamu.

Bi. Mohammed amezungumzia pia suala la ubakaji nchini Sudan Kusini akisema ni lazima lishughulikiwe kwa kuwa, “hata ghasia kwa mwanamke mmoja ni ghasia kwa wanawake wengi.”

Amesema amani ni muhimu zaidi wakati huu na ni lazima iwe jumuishi kwa kadri inavyowezekana na amekaribisha mkakati wa Khartoum unaotokana na mazungumzo kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na kiongozi wa upinzani Riek Machar.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (wa kati kulia) akizungumza na wanahabari mjini Juba, Sudan Kusini. Kulia kwake ni Bineta Diop, mjumbe maalum wa AU kwa masuala ya Wanawake, Amani na Usalama.
UN/Isaac Billy
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (wa kati kulia) akizungumza na wanahabari mjini Juba, Sudan Kusini. Kulia kwake ni Bineta Diop, mjumbe maalum wa AU kwa masuala ya Wanawake, Amani na Usalama.

Naibu Katibu Mkuu aliambatana na Bineta Diop, mjumbe maalum wa Muungano wa Afrika kwa masuala ya wanawake, amani na usalama ambaye amesema wanawake lazima wasongeshe ajenda ya amani nchini humo.

“Uwajibikaji unahitajika, huduma za kisheria zinahitajika maeneo ya vijijini iwapo haki haitapatikana mashinani, basi ujenzi wa amani hautafanikiwa,” amesema Bi. Diop.

Hivi karibuni Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na kiongozi wa upinzani Riek Machar walikutana mjini Khartoum nchini Sudan na kuelezea azma yao ya kusaka suluhu ya mzozo nchini mwao.

Mapigano nchini Sudan Kusini yalianza mwezi disemba mwaka 2013 na hadi sasa yamesababisha mamia ya maelfu ya raia kukimbia makazi yao na kusaka hifadhi maeneo mengine ya nchi na hata nchi jirani.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter