Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusiwatupe mkono wapalestina -Guterres

Mechi ya kirafiki kati ya wafanyakazi wa UNRWA dhidi ya wakimbizi wa Palestina Gaza mapema 2018
UNRWA
Mechi ya kirafiki kati ya wafanyakazi wa UNRWA dhidi ya wakimbizi wa Palestina Gaza mapema 2018

Tusiwatupe mkono wapalestina -Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Ni lazima tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa chakula kinaendelea kufikia wapalestina na shule zinabaki zimefunguliwa  na pia watu wasikate tamaa.

Hayo yametamkwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika mkutano wa leo uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York nchini Marekani kwa ajili ya kuchangisha fedha kusaidia shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA.

Bw. Guterres  amewaeleza washiriki kuwa UNRWA inahitaji msaada kwani kazi zake zinashughulikia kumaliza njaa pamoja na elimu kwa watoto wa wakimbizi wa kipalestina.

(SAUTI YA GUTERRES)

“ Kwa miongo kadhaa, elimu ya UNRWA imeweka kiwango kwa eneo zima. Usawa wa kijinsia umekuwa ndio kawaida  katika shule na pia mafanikio popote pale na pia katika eneo ambalo limekuwa kipambana na suala hili”

 Ameendelea kuwa  msaada wa chakula ambao UNRWA inatoa kwa wakimbizi milioni 1.7 wa kipalestina unazuia njaa , na kuongeza kuwa shirika hilo hufanya hayo yote katika mazingira magumu ya  kiuchumi na pia kutokana na mgogoro wenyewe unaoendelea.

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) Akihutubia mkutano kuhusu hatua za pamoja kusaidia UNRWA
FAO/Pier Paolo Cito
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) Akihutubia mkutano kuhusu hatua za pamoja kusaidia UNRWA

Katibu Mkuu amesema UNRWA imechukua hatua kadhaa ili kuendelea kusaidia wakimbizi wa kipalestina..

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Lakini juhudi hizo hazitatosha kufadhili kikamilifu pengo lililopo mwaka huu. Tutategemea wanachama wa Umoja wa Mataifa kuziba pengo hilo.”

Naye Kamishna mkuu wa UNRWA Pierre Krahenbuhl, amesema wanakabiliwa na ukata ambao haujawahi kushuhudiwa kutokana na kujiondoa kwa mfadhili mkuu Marekani, akisema pengo lililojitokeza ni la asilimia 32.

Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu huyo wa UNRWA amesema wakimbizi wa kipalestina wanahisi wametengwa.

(SAUTI YA PIERRE KRAHENBUHL)

 “Kwanza kwa  sababu Wakimbizi wa Kipalestina hawaoni suluhu ya shida zao.  Sasa ni zaidi ya miaka 20 tangu  mkataba wa amani wa Oslo, na kizazi ambacho kimezaliwa tangu wakati huo ambacho ndio sehemu kubwa ya idadi ya wakimbizi hao hawaoni muafaka ukifikiwa siku za hivi karibuni kisiasa au kibnafsi.”

Amesema kati ya wanafunzi 52,000 wanaowahudumia, elfu 27 wako ukanda wa Gaza na asilimia 90 kati yao hao hawajaondoka kutoka ukanda huo.

Bwana Krahenbuhl amesema ni kwa mantiki hiyo wanaomba msaada wa kifedha kuweza kuwahudumia watoto hao na wakimbizi wengine.