Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi yaleta zahma kwa mamilioni 2017:UN

Patricia Espiona, Katibu Mtendaji wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusu mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) katika mkutano wa Tabianchi Bonn Ujerumani
UNFCCC
Patricia Espiona, Katibu Mtendaji wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusu mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) katika mkutano wa Tabianchi Bonn Ujerumani

Mabadiliko ya tabianchi yaleta zahma kwa mamilioni 2017:UN

Tabianchi na mazingira

Mwaka wa 2017 umeelezwa kama ulioshudia matukio yaliyofurutu ada ya hali ya hewa na hivyo kuwafanya mamilioni ya watu duniani kuteseka. Hivyo Umoja wa Mataifa unasema si hadhithi tena bali athari za mabadiliko ya tabia nchi zimeanza kushudiwa hususan katika jamii zilizo hatarini zaidi.

Hayo yametamkwa na mkuu wa idara inayohusika na mabadiliko ya tabianchi kwenye Umoja wa Mataifa UNFCCC, Bi. Patricia Espinosa, wakati wa kuanza kwa  mkutano kuhusu  mabadiliko ya tabianchi mjini Bonn Ujerumani.


Mkutano huu ambao umeanza leo Jumatatu Aprili 30 na kutarajiwa kumalizika Mei 10 mwaka 2018, unawahusisha wajumbe  wa serikali kutoka nchi mbalimbali ambao wanajaribu kuona jinsi gani ya kuharakisha utekelezwaji wa makubaliano ya Paris ya mwaka 2015, kuhusu mabadiliko ya tabianchi.


Bi Espinosa ameongeza kuwa ili kufanikisha mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi wa COP24, ni muhimu mataifa yakaanza sasa kupanga mambo yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo. Amesema kuwa hii itaunda msingi wa kazi za awamu ya pili ya mwaka 2018 na kusaidia kutoa matokeo mazuri.


Matokeo ya mkutano wa Bonn ni muhimu mno kwani yataondoa mikingamo ya kuweka vitendoni hatua za kutekeleza mkataba wa Paris. Maamuzi ya mwisho ni mwishoni mwa mwaka huu katika mkutano wa COP24 -utakaofanyika nchini Poland.


Kukamilisha mwongozo wa mkataba wa Paris pia  ni muhimu ili kutathmini ikiwa  dunia inafuata dira  ya kupata  malengo ya mkataba, ambayo miongoni mwa mengine, ni kupunguza joto hadi nyuzi joto 2 huku ikipambana kuona kama  inaweza ikasalia kwenye nyuzi- joto  1.5.