Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu mpya za pamoja zitawezesha kukabili kitisho cha ugaidi

Raia katika mji wa Mosul, Iraq baada ya shambulio la gari la  kujitoa mhanga.
© UNHCR/Ivor Prickett
Raia katika mji wa Mosul, Iraq baada ya shambulio la gari la kujitoa mhanga.

Mbinu mpya za pamoja zitawezesha kukabili kitisho cha ugaidi

Amani na Usalama

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi, Vladimir Voronkov, amesema suala ya kwamba ugaidi unaendelea kuwa tishio la amani na usalama duniani linahitaji siyo tu kufuatiliwa na Baraza la Usalama bali pia mbinu mpya za pamoja kama iliyoelezwa na Katibu Mkuu Antonio Guterres kwenye Ajenda yake ya Pamoja. 

Ajenda mpya ya amani kutoa majawabu- Vonkorov 

Akihutubia Baraza la Usalama hii leo lililokutana kujadili Mbinu Mpya ya kimataifa ya kupambana na tishio la ugaidi kwenye amani na usalama duniani, Bwana Vonkorov amesema Ajenda Mpya ya Amani itakayotolewa na Katibu Mkuu italenga kushughulikia vitisho  vya amani vinavyotangamana  ambavyo si tu ugaidi bali pia mapigano, hali mbaya ya madhara ya tabianchi, umaskini, ukosefu wa usawa, majukwaa ya mtandaoni yasiyodhibitiwa na ukosefu wa usawa. 

Amesema ni kwa mantiki hiyo amesisitiza wito wa Bwana Guterres wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa kama suala la lazima na si chaguo kwa sababu ni muhimu katika kukabili ugaidi ambao amesema licha ya baadhi ya vikundi kupoteza viongozi wao, bado makundi yanazidi kusambaa akitolea mfano AlQaeda na Da’esh. 

Bwana Vonkorov amesema makundi hayo yanatumia changamoto zinazokabili jamii kusambaza mikakati yao akitolea mfano Afrika Magharibi, na Sahel ambapo hali ni ya dharura. 

Amepongeza azimio la New Delhi lililopitishwa na Kamati ya Baraza la Usalama la kukabili ugaidi, CTED akisema ni njia sahihi kuelekea kukabili ugaidi duniani. 

Menaka kaskazini mashariki mwa Mali imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi na makundi mengine yenye silaha.
MINUSMA/Gema Cortes
Menaka kaskazini mashariki mwa Mali imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi na makundi mengine yenye silaha.

Uwanda wa kigaidi unazidi kupanusha na kushamiri- Chen 

Naye Weixiong Chen, Kaimu Mkurugenzi wa Kamati tendaji ya Kamati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kukabili ugaidi, CTED, akihutubia mkutano huo amesema uwanda wa kigaidi unazidi kupanuka na kubadilika kila uchao huku magaidi wakiendelea kuboresha mbinu na mikakati yao. 

Bwana Chen ametaja vikundi vya Da’esh, AlQaeda na washirika wao ambao amesema vinazidi kujiimarisha mashinani na vitisho vinazidi kubadilika na kupanuka akisema kando mwa maeneo yao walikozoeleka, viwanja vya mapambano vimeibuka Ukanda wa Sahel, Afrika Magharibi, Kusini, Mashariki na Kati bila kusahau baadhi ya maeneo ya Asia. 

Vitisho vya ugaidi vinazidi kusambaa 

 “Tunashuhudia pia ongezeko la vitisho vya ugaidi kwa misingi ya chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na aina nyingine za ukosefu wa stahmala. Vikundi hivi vinavuka hata na mipaka sasa,” amesema Bwana Chen. 

Amesema pamoja na kuimarisha mtandao wao kwa kuvuka mipaka vikundi hivyo vinachochea misimamo mikali huku vikitoa usaidizi wa fedha na operesheni za ugaidi,  

Magaidi pia wanaendelea kutumia majukwaa mtandaoni mathalani majukwaa ya michezo mtandao kutumikisha na kujenga misimamo mikali, kuchangisha fedha na kuratibu operesheni zao halikadhalika kusambaza propaganda zao. 

Ni kwa kutambua hilo, amesema Bwana Chen, Kamati ya Baraza la Usalama ya kukabili ugaidi ilikuwa na kikao maalum nchini India mwezi Oktoba mwaka huu na kujadili mbinu za kukabili aina mpya za teknolojia zinazotumiwa na magaidi na kupitisha Azimio la New Dheli linalosisitiza ushirikiano nan chi wanachama katika kutekeleza maazimio ya Baraza ya kushughulikia vitisho vya ugaidi. 

Bwana Chen amesema, “kufanikisha malengo yetu, lazima tufanye kazi pamoja kwa njia ya ushirikiano, tukihusisha wadau kwa mapana na kwa wingi zaidi zikiwemo nchi wanachama, mashirika ya kimataifa na kikanda, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.”