Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wafanya nini kukabili janga la wakimbizi?

Genesis Cerrato, mwenye umri wa miaka 16 akiwa na mwanae wa kiume mwenye umri wa mwaka  mmoja. Genesis na familia yake yote walikimbia nchi yao Mexico na kuingia Honduras kwa hofu ya ghasia nchini mwao.
UNHCR/Markel Redondo
Genesis Cerrato, mwenye umri wa miaka 16 akiwa na mwanae wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja. Genesis na familia yake yote walikimbia nchi yao Mexico na kuingia Honduras kwa hofu ya ghasia nchini mwao.

Je wafanya nini kukabili janga la wakimbizi?

Wahamiaji na Wakimbizi

Ungalifanya nini iwapo ungelazimishwa kuondoka nyumbani kwako?

Hivyo ndivyo unavyoanza ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika siku ya wakimbizi duniani hii leo.

Yaelezwa kuwa hadi sasa zaidi ya watu milioni 68 ni wakimbizi ugenini au ndani ya nchi zao, sababu kuu ikiwa ni mizozo au mateso kwenye nchi zao.

Katibu Mkuu anasema idadi hiyo ni sawa na idadi ya watu kwenye nchi ya 20 kwa ukubwa zaidi duniani. “Mwaka jana, katika kila sekunde mbili mtu mmoja alikimbia makazi. Hasa katika nchi maskini zaidi,” amesema Guterres.

Kwa mantiki hiyo katika siku ya Wakimbizi Duniani, hii leo anasema ni “lazima tufikirie tufanye nini zaidi ili kusaidia. Jibu linaanza na umoja na mshikamano.”

Hata hivyo linalomtia shaka zaidi, “nina wasiwasi mkubwa kushuhudia mazingira zaidi ambamo wakimbizi hawapati ulinzi wanaohitaji na ambao ni haki yao. Tunahitaji kuanzisha tena maadili ya mfumo wa kimataifa wa ulinzi wa wakimbizi.”

Maher Bajjur, mkimbizi kutoka Syria ambaye sasa amepata hifadhi nchini Argentina ambako anaishi na kaka yake Tamer kwenye jimbo la San Luis.
UNIC Buenos Aires
Maher Bajjur, mkimbizi kutoka Syria ambaye sasa amepata hifadhi nchini Argentina ambako anaishi na kaka yake Tamer kwenye jimbo la San Luis.

Bwana Guterres anasema katika dunia ya leo jamii au nchi ambayo inayotoa hifadhi salama kwa wakimbizi wanaokimbia vita au mateso hawapaswi kuachwa peke  yao bila kusaidiwa.

Kwa mantiki hiyo anasema jambo muhimu sasa ni kuamua kuungana na kuwa kitu kimoja au kutengana na kuporomoka.

Amepigia chepuo mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi utakaowasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baadaye mwaka huu akisema unatoa mwelekeo wa mbele na kutambua michango ya wakimbizi katika jamii zinazowahifadhi.

“Alimradi kuna vita na mateso, wakimbizi wataendelea kuwepo.   Katika siku ya Wakimbizi Duniani, nakuomba uwakumbuke. Simulizi zao ni za mnepo, uvumilivu na ujasiri. Zetu zinapaswa kuwa za mshikamano, upendo na vitendo.” Amehitimisha Katibu Mkuu.

Ungalifukuzwa kwako ungalifanya nini?