Ujasiriamali ni daraja kati ya wakimbizi, wahamiaji na jamii:UN

25 Oktoba 2018

Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa yamezindua mwongozo wa sera mpya kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi na wahamiaji, wadau wa maendeleo na washirika wa kibinadamu, utakaosaidia kujenga fursa za kiuchumi kwa wahamiaji na wakimbizi.

Mwongozo wa sera hiyo mpya unaoyahusisha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM na kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara UNCTAD , umezinduliwa kwenye kongamano la la kimataifa la uwekezaji linalofanyika mjini Geneva Uswis.

Mashirika hayo yanasema moja ya fursa kubwa ya kufanikisha azma hiyo ni ujasiriamali ambao una uwezo wa kuweka mazingira ya faida kwa pande zote, yaani kwa wakimbizi na wahamiaji na nchi zinazowahifadhi.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, sera hiyo mpya inatoa mwongozo kwa vitendo kwa nchi zinazohifadhi wahamiaji na wakimbizi , wadau wa maendeleo na wa misaada ya kibinadamu,  wa jinsi gani ya kuhakikisha kwamba wakimbizi na wahamiaji wanatumia ujuzi na uwezo walionao kujenga maisha yao na wakati huohuo kuchangia katika jamii zinazowahifandi na uchumi.

Akisisitiza umuhimu wa kutoa fursa hizo za ujasiriamali kwa wakimbizi na wahamiaji , naibu katibu mkuu wa UNCTAD Isabelle Durant amesema “kuunda fursa za kiuchumi kwa wote kwa lengo la kuhakikisha hakuna anayesalia nyuma ni kipaumbele cha ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030, na njia mojawapo ya kufanikisha hili ni kupitia uchagizaji wa ujasiriamali.”

Mashirika hayo matatu yakizichagiza nchi kushikamana nao katika mkakati huu mpya yamesema ujasiriliamali unaweza pia kuwa suluhu ya kudumu inayohitajika kushughulikia changamoto za wimbi kubwa la watu wanaolazimika kukimbia makwao, ukienda sanjari na hatua zingine muhimu ambazo tayari zimeshawekwa kushughulikia athari za mgogoro wa kibinadamu unaotokana na wimbi la wahamiaji na wakimbizi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter