Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya mafanikio makubwa Rio, sasa mwelekeo Tokyo 2020

Mmoja wa wakimbizi kutoka Syria ambaye alishiriki mashindano ya Rio 2016, Rami Anis wakati wa mazoezi huko Ghent, Ubelgiji
UNHCR/Gordon Welters
Mmoja wa wakimbizi kutoka Syria ambaye alishiriki mashindano ya Rio 2016, Rami Anis wakati wa mazoezi huko Ghent, Ubelgiji

Baada ya mafanikio makubwa Rio, sasa mwelekeo Tokyo 2020

Wahamiaji na Wakimbizi

Sasa imethibitishwa kuwa wanamichezo wakimbizi watashiriki katika mashindano ya olimpiki huko Tokyo Japan mwaka 2020.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hatua hiyo inafuatia  mafanikio makubwa ya wanamichezo hao katika mashindano yaliyofanyika huko Rio nchini Brazil mwaka 2016.

Uamuzi umetangazwa katika kikao cha 133 cha kamati ya kimataifa ya olimpiki, IOC kilichokutana jumanne huko Buenos Aires nchini Argentina.

Akihutubia kikao  hicho kabla ya kura ya uamuzi, Yeir Pur Biel ambaye ni muungaji mkono wa ngazi ya juu wa UNHCR na pia  mmoja wa wanamichezo waliowakilisha wakimbizi huko Rio alitaka wajumbe kutumia fursa ya kipekee ya kuendeleza kile ambacho tayari kimefanikiwa na kuwa na timu ya pili ya wakimbizi huko Tokyo 2020.

Tangu mashindano ya zama mpya ya olimpiki yaanze mwaka 1896, zaidi ya timu za mataifa 200 zimeshiriki michezo hiyo na ilikuwa mara ya kwanza mwaka 2016 kwa timu ya wakimbizi kushiriki.

Timu hiyo ilihusisha wakimbizi 10 kutoka nchi nne na miongoni mwao waogeleaji wawili, wacheza judo wawili, mkimbiaji mmoja wa mbio ndefu za marathoni na wakimbiaji watano wa mbio za umbali wa kati.

Uamuzi huo wa wakimbizi kushiriki mashindano ya Tokyo umekaribishwa na kamishna mkuu wa UNHCR Filippo Grandi akisema “mwaka 2016, timu ya wakimbizi huko Rio ilinasa fikra za watu kote duniani na kuwaonyesha upande mwingine wa kibinadamu wa janga la wakimbizi kupitia michezo.”

Amesema amefurahishwa sana kwa utamaduni huo kuendelezwa Tokyo akisema kuwapatia vijana fursa hiyo ya kipekee kushiriki kwenye michezo ni jambo la kuvutia sana.