Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hifadhi ya ukimbizi wangu iko katika soka:Abdi

Vijana wakimbizi wapata kimbilio kwenye soka
IOM 2018/Ahmed Badr
Vijana wakimbizi wapata kimbilio kwenye soka

Hifadhi ya ukimbizi wangu iko katika soka:Abdi

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati michuano ya kombe la dunia iking’oa nanga hii leo nchini Urusi na kukutanisha mamilioni ya watu, vijana barubaru wakimbizi kutoka Afrika mashariki waishio hapa Marekani wamesema kabumbu imewasahaulisha ukimbizi .

Michezo inafahamika kwa kujumisha watu pamoja licha ya dini, rangi au watokako, kuanza kwa kombe la dunia la soka hii leo huko Urusi kumewahamasisha vijana barubaru wakimbizi wenye asili ya Kisomali  kutoka Afrika Mashariki ambao wanasakata kabumbu mjini salt Lake City Utah hapa nchini Marekani.

Wanaamini kwamba michezo huburudisha lakini pia husaidia kuliwaza waliopitia masahibu kama kijana wa Mohammed Abbas Abdi mwenye umri wa miaka 21.

Alikulia mkimbizi  na alikulia kambini  Mombasa nchini Kenya alipofikisha miaka 13 wazazi wake walipata hifadhi ya ukimbizi Marekani hivi sasa pamoja naye wanaishi Salt Lake City.

Anasema “Maisha ni kama kabumbu, unachotakiwa ni kulisakata kkwa nguvu zote  na utafanikiwa” na ndicho kilichomsaidia yeye na vijana wengine barubaru kutoka Afrika Mashariki kukabiliana na changamoto na mabadiliko waliyopitia kwenye na kujikumbusha nyumbani Kenya waliokuwa wakisakata mpira wa miguu uliotengenezwa na makaratasi ya plastiki.

Vijana hao wote wako kwenye timu ya soka yenye maskani yake Utah na kushiriki soka pia kumewasaidia kuchangamana na wenjeji na kujihisi sio wakimbizi tena ,wanajifunza utamaduni mpya, wanajipatia marafiki na fursa ambazo ilikuwa vigumu walipokuwa wakimbizi Afrika.

Abdi na wenzie wameiambia timu ya Umoja wa Mataifa ya kampeni ya kuchagiza usalama, utu na heshima kwa wakimbizi na wahamiaji  kwamba vijana walio katika madhila wakishiriki michezo itasaidia kuwapunguzia machungu.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM hivi sasa kuna Zaidi ya wakimbizi, wahamiaji, waomba hifadhi na wakimbizi wa ndani milioni 65 kote duniani.