DPRK achia huru wafungwa wa kisiasa kabla ya mkutano na Marekani-UN

7 Juni 2018

Kuelekea mkutano wa viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini nchini Singapore, UN yapaza sauti ili mazungumzo hayo yawe na manufaa zaidi.

Umoja wa Mataifa umeitaka Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK iachilie kwanza huru wafugwa wa kisiasa kabla ya mazungumzo yake na Marekani kuhusu kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini DPRK, Tomas Ojea Quintana amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi akizungumza na waandishi wa habari.

Amepongeza hatua ya kuachiliwa huru kwa wafungwa watatu wa kimarekani kutoka DPRK mwezi uliopita lakini anataka hatua zaidi kuachilia huru wafungwa wengine waliokamatwa kiholela nchini humo kwa msingi wa kisiasa.

Bwana Quintana amefafanua kuwa ombi lake la kutaka wafungwa hao wa kisiasa waachiliwe huru si kwamba anataka litekelezwe kwa ghafla tu bali liwe ni mchakato unaofuata kanuni.

Idadi kamili ya wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa DPRK, ijulikanayo pia kama Korea Kaskazini bado haifahamiki, lakini mtaalamu huyo ambaye bado hajapata fursa ya kutembelea nchi hiyo amesema inawezekana idadi yao ni zaidi ya 80,000.

Mkutano kati ya viongozi wa DPRK na Marekani unatarajiwa kufanyika nchini  Singapore katika lengo la kuishawishi nchi hiyo ya barani Asia iachane na mpango wake wa nyuklia.

“Ili mazungumzo hayo yaweze kuwa na matunda ni lazima haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni za raia zijumuishwe,” amesema Bwana Quintana akiongeza kuwa mazungumzo ya awali hayajaweza kuzaa matunda kwa kwa mambo hayo hayakujumuishwa.

Ametaja makubaliano na DPRK yam waka 1994 na mazungumzo ya pande sita yam waka 2003 ambayo amesema ingawa yalionekana kuwa na nia njema, hayakuzaa matunda.

Mtaalamu huyo amesema ili mazungumzo hayo ya tarehe 12 mwezi huu yawe na manufaa hoja ya haki za binadamu nayo pia iunganishwe kwa sababu haki za binadamu ni jambo linaloenda pamoja na amani na usalama

Nchini DPRK zaidi ya watu milioni 10 wanahitaji misaada ya kibinadamu wakati huu ambapo ombi la Umoja wa Mataifa la dola milioni 12 la kufanikisha msaada huo bado halijafadhiliwa vya kutosha.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter