Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa raia vitani- maneno mengi kuliko vitendo

Nchini Yemen kusambaratika kwa miundombinu ya afya na ile ya  majisafi na majitaka kumesababisha kazi ya kukabili magonjwa kuwa ya shida.
UNICEF/UN065871/Alzekri
Nchini Yemen kusambaratika kwa miundombinu ya afya na ile ya majisafi na majitaka kumesababisha kazi ya kukabili magonjwa kuwa ya shida.

Ulinzi wa raia vitani- maneno mengi kuliko vitendo

Amani na Usalama

Mizozo kote duniani inaibua vitisho na machungu kwa mamilioni ya raia wakiwemo wanawake, wasichana, wanaume, wavulana na watoto.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kilichokutana hii leo jijini New York, Marekani kujadili ulinzi wa raia kwenye mizozo ya kivita.

Guterres amesema zaidi ya watu milioni 128 kote ulimwengni wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu na idadi hii kubwa inatokana na mizozo.

“Mwaka jana Umoja wa Mataifa ulirekodi vifo na majeruhi zaidi ya 26,000 miongoni mwa raia katika nchi sita tu zilizoathiriwa na mizozo duniani,” amesema Katibu Mkuu akizitaja nchi hizo kuw ani Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Iraq, Somalia na Yemen.

Katibu Mkuu amesema kama hiyo haitoshi, raia hao hao kwenye maeneo ya mizozo wanakumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo kubwaka na aina nyingine za ukatili wa kingono.

 

Watoto katika kijiji cha Benakuna, Kasai DRC.Watoto kama hao hunyanyaswa wakati wa migogoro.
UNICEF/Vincent Tremeau
Watoto katika kijiji cha Benakuna, Kasai DRC.Watoto kama hao hunyanyaswa wakati wa migogoro.

Ametolea mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akisema “Umoja wa Mataifa ulirekodi zaidi ya visa 800 vya ukatili wa kingono unaohusiana na kuwepo kwa mzizo, ambapo ni ongezeko kwa asilimia 56 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia,” amesema Guterres.

Kando mwa ukatili wa kingono, vifo na majeruhi, mizozo imeendelea kuwaong’oa watu kutoka kwenye makazi yao na kusalia bila kufahamu mustakhbali wao.

"Mwishoni mwa mwaka 2016, zaidi ya watu milioni 65 walikuwa ni wakimbizi kutokana na kukimbia mizozo, mateso na ghasia. Wengine wengi hawajulikani waliko,” ameongeza Katibu Mkuu.

Bwana Guterres akatumia fursa hiyo basi kupazia sauti vitendo vya pande kinzani kwenye mizozo kuangusha au kufyatua makombora yao kwenye makazi ya watu kinyume na sheria za haki za kimataifa za kibinadamu.

Mashambulizi hayo kwenye miji na majiji amesema, “ yanaua na kujeruhiwa makumi ya maelfu ya raia kila mwaka, na kusambaratisha makazi na miundombinu muhimu ikiwemo ile ya maji na nishati.”

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametoa mapendekezo matatu, mosi serikali zitunge sera za kitaifa za kulinda raia kwenye mizozo, pili nchi wanachama ziunge mkono Umoja wa Mataifa na wadau wengine katika kushirikiana na vikundi visivyo vya kiserikali kutunga sera, mifumo na mipango ya kulinda raia.

 

Pendekezo la tatu ni kwamba nchi wanachama ziunge mkono uchechemuzi wa kulinda raia na kuchukua hatua za pamoja kuhakikisha uwajibikaji kwa wahusika ili kuepusha ukwepaji sheria.

Wajumbe wa Baraza la Usalama walisikiliza pia hotuba kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la msalaba mwekundu duniani, ICRC Yves Daccord ambaye amesema cha kusikitisha sera za kulinda raia kwenye mizozo haziendani na kile kinachoandelea kwenye uwanja wa mapambano.

Anasema wanachoshuhudia ni mambo lukuki ikiwemo mtoto aliyeshambuliwa na kuachwa yatima baada ya wazzi wake kuuawa, majela yaliyojaa pomoni bila mifumo bora ya ulinzi wa wafungwa.

“Jinsi ya kuondoa pengo kati ya maneno ya vitendo ni ujumbe rahisi sana, ni kuzingatia msingi wa ubinadamu. Sheria ya kimataifa ya kibinadamu, IHL. Sheria hii imetungwa kuheshimu na kulinda ubinadamu na utu," amesema mkuu huyo wa ICRC.