Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maneno tu bila vitendo hayatasaidia ushiriki wa wanawake kwenye  ujenzi wa amani- Guterres

Walinda amani wanawake wana mchango mkubwa katika kusaidia kurejesha amani na kujenga amani ya kudumu kwenye maeneo ya mizozo. Pichani ni walinda amani kutoka Afrika Kusini walioko DR Congo
MONUSCO
Walinda amani wanawake wana mchango mkubwa katika kusaidia kurejesha amani na kujenga amani ya kudumu kwenye maeneo ya mizozo. Pichani ni walinda amani kutoka Afrika Kusini walioko DR Congo

Maneno tu bila vitendo hayatasaidia ushiriki wa wanawake kwenye  ujenzi wa amani- Guterres

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wake wa wazi wa kila mwaka kuhusu wanawake, amani na usalama likiangazia zaidi jinsi uwezeshaji wanawake kiuchumi na kisiasa kunaweza kuimarisha amani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi nchi wanachama ziwekeze zaidi katika usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kama njia mojawapo ya kufanikisha lengo la kumaliza mizozo, kujenga amani ya kudumu na ustawi wa kila mkazi wa dunia.

Guterres amesema hayo wakati wa mjadala wa wazi wa kila mwaka wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika jijini New York, Marekani hii leo ukiangazia zaidi jinsi uwezeshaji wanawake kiuchumi na kisiasa unaweza kuimarisha amani.

Katibu Mkuu amesema ni vyema kurejelea wito huo kwa sababu “tumekuwa mstari wa mbele kupaza sauti juu ya  umuhimu wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake huku tukikata bajeti za kuwezesha mipango hiyo.”

Amesema kila mwaka tunaweka ahadi nzito lakini haziungwi mkono ipasavyo kisiasa na kifedha na zaidi ya yote, “tunarudia takwimu kuhusu michakato ya amani iliyo endelevu na jumuishi, lakini mara nyingi hivyo sivyo ambavyo tunasuluhisha mizozo,” akiongeza kuwa uchambuzi wa kijinsia ni muhimu katika kutumia fursa hiyo kuleta amani ya kudumu, “lakini tunakata bajeti za kuwezesha utaalamu huo.”

Kwa hivyo Bwana Guterres amesema ili kushughulikia pengo hilo katika mwaka ujao atapatia kipaumbele mambo matano  ikiwemo mosi, usawa wa kijinsia kwenye operesheni za Umoja wa Mataifa, “wanawake sasa ni asilimia 41 ya wakuu na naibu wa operesheni zetu za ulinzi wa amani.”

Ushirikiano baina ya wanawake ni muarobaini wa maendeleo hata kule mashinani kama inavyoonekana pichani walinda amani wanawake huko Darfur, Sudan wakielekeza wanawake mapishi ya maandazi.
UN /Muntasir Sharafdin
Ushirikiano baina ya wanawake ni muarobaini wa maendeleo hata kule mashinani kama inavyoonekana pichani walinda amani wanawake huko Darfur, Sudan wakielekeza wanawake mapishi ya maandazi.

Pili, amesema ni kushirikisha wanawake kwenye mchakato wa usuluhishi akisema “kuanzishwa kwa mitandao mingi ya wanawake hivi karibuni ni mwelekeo mzuri na wanaweza kuwa na dhima shawishi katika kufanya michakato iwe bora zaidi.”

Kipaumbele kingine ni kusaidia ujenzi wa amani mashinani hata wakati wa mizozo akisema, hata pale michakato ya amani inaposhamiri kitaifa na kimataifani lazima kusaidia wanawake walioko mashinani ambao kwa njia moja au nyingine wanasongesha amani.

Kipaumbele cha nne ni kufadhili ajenda ya ushiriki wa wanawake akisema “Umoja wa Mataifa unalenga kuongoza kwa mfano. Nimeunda kikosi kazi cha ngazi ya juu kutathmini ufadhili wetu kwenye masuala ya jinsia ikiwemo nyanja ya amani na usalama."

Tunarudia takwimu kuhusu michakato ya amani iliyo endelevu na jumuishi, lakini mara nyingi hivyo sivyo ambavyo tunasuluhisha mizozo. Tunataka utaalamu wa uchambuzi wa kijinsia lakini tunakata bajeti za kuwezesha utaalamu huo. 

Na hatimaye Katibu Mkuu akaahidi kuwa kuanzia sasa ripoti zake zote atakazowasilisha Baraza la Usalama zitakuwa na uchambuzi wa kijinsia ili kuwezesha kusaidia maamuzi yaliyo sahihi katika ajenda ya ushiriki wa wanawake kwenye amani na usalama duniani.