Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajibu wa kulinda ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akizungumza katika mjadala wa wazi wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuhusu wajibu wa kulinda maisha ya watu.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akizungumza katika mjadala wa wazi wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuhusu wajibu wa kulinda maisha ya watu.

Wajibu wa kulinda ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote:Guterres

Amani na Usalama

Majadiliano kuhusu wajibu wa kulinda maisha ya watu ni muhimu sana leo hii kuliko wakati mwingine wowote, wakati dunia ikijitahidi kwa pamoja kuwalinda watu  hao dhidi ya  mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita, mauaji ya kikabila na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akizungumza katika mjadala wa wazi wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuhusu wajibu wa kulinda maisha ya watu , uliopitishwa kwa kauli moja na viongozi wa dunia mwaka 2005 baada ya kushuhudia mauaji ya kimbari ya Rwanda na Sebrenica. Lengo likiwa bayana amesema kuongeza juhudi kwa pamoja kama jumuiya ya kimataifa kuwalinda watu hao.

“Hata hivyo leo hii bado kuna hofu kwamba kanuni hiyo inaweza kutumika kuchukua hatua ya pamoja kwa madhumuni mengine kuliko yale yaliyoafikiwa katika matokeo ya mkutano wa dunia. Pia kuna wasiwasi juu ya viwango vya pande mbili na matumizi ya kuchagua ya kanuni hizo katika siku za nyuma.”

Na hii ndio sababu amesema uwazi katika kujadili suala hili ni lazima, ili  kuondokana na hisia zisizo sahihi  na kutoaminiana akihimiza “Tunapaswa kuunda uelewa wa pamoja na kutoa msaada mkubwa kwa wajibu huu, kama chombo muhimu cha ulinzi na kuzuia maafa.”

Image
UN News Center
Vijana husambaratishwa na migogoro nchini DRC. Picha: UN News Center

Guterres amesisitiza kwamba kulinda raia ni wajibu wa kila taifa na kwa mukhtada huo ripoti yake safari hii imependekeza hatua kadhaa ambazo nchi itazichukua ili kuimarisha uwezo wake katika wajibu huu

“Zikijumuisha kufanya tathimini za kitaifa za hatari na kuunda sera za kukabiliana na udhaifu wowote, kupanua wigo wa ushiriki wa asasi za kiraia pia ni muhimu katika kutoa tahadhari ya mapema na kuhakikisha utendaji wa taasisi za kitaifa za haki za binadamu, na pia nazichagiza nchi wanachama kuridhia na kuzitekeleza nyumbani searia za kimataifa ambazo zinahusiana na kukataza na kuzuia uhalifu na ukiukaji ulioainishwa kwenye matokeo ya mkutano.”

Hadi kufikia sasa nchi wanachama 45 bado hazijaridhia mkataba kuhusu kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari. Ameikumbusha jumuiya ya kimataifa kuwa ina jukumu la kuzisaidia nchi kutekeleza wajibu huo. Ameongeza kwamba ingawa dunia sasa hivi inashuhudia madhila na ukatili uliofurutu ada lakini

Eneo la Yambio nchini Sudan Kusini, watoto hawa wawili wakiwa wameshikana mabegani wakielekea eneo salama baada ya kuachiliwa huru kutoka makundi yaliyojihami ambayo yalikuwa yanawatumikisha vitani.
UNICEF/UN0202141/Rich
Eneo la Yambio nchini Sudan Kusini, watoto hawa wawili wakiwa wameshikana mabegani wakielekea eneo salama baada ya kuachiliwa huru kutoka makundi yaliyojihami ambayo yalikuwa yanawatumikisha vitani.

“Hakuna uhalifu kama huu usioepukika au matokeo ya migogoro. Uhalifu wote wa kikatikli unazuilika na hauwezi kamwe kuhalalishwa. Hii ilikuwa sababu ya barua yangu rasmi kwa Baraza la Usalama Agosti mwaka jana kuhusu zahma ya Rohingya nchini Myanmar.”

Ametaja changamoto kubwa hivi sasa “ni kuzingatia kanuni huku tukizuia matumizi mabaya ya kanuni hizo, hii ikimaanisha ni kuchukua hatua haraka, kuzuia na kwa njia ya kidiplomasia, kabla hali haijawa mbaya zaidi  na kushindwa kuidhibitika, kwani mustakhbali wa mamilioni ya watu uko mikononi mwetu.