Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hebu tuchukue hatua ili maliasili zisiwe kichocheo cha mizozo- Guterres

Uthibitishaji wa magogo ni njia mojawapo ya kuepusha maliasili hii kutumiwa katika kuchochea mizozo, Hapa ni DR Congo katika bohari la kuhifadhi magogo.
Flore de Preneuf/World Bank/FP-DRC-4490
Uthibitishaji wa magogo ni njia mojawapo ya kuepusha maliasili hii kutumiwa katika kuchochea mizozo, Hapa ni DR Congo katika bohari la kuhifadhi magogo.

Hebu tuchukue hatua ili maliasili zisiwe kichocheo cha mizozo- Guterres

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala kuhusu uendelezaji wa amani na usalama duniani, mwelekezo zaidi ukiwa ni dhima ya maliasili kama vile mafuta na madini katika kusababisha mizozo na mapigano.

 Akihutubia mkutano huo ulioitishwa na Bolivia ambayo ndiyo rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Oktoba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni dhahiri shairi kuwa utafutaji wa rasilimali hizo pamoja na mashindano ya kuzimiliki vinaweza na husababisha mapigano makali.

Hata hivyo amesema “kuzuia, kusimamia na kutatua mizozo itokanayo na ugombeaji wa maliasili hizi ni moja ya changamoto kubwa zaidi kwa zama za sasa,” akiongeza kuwa “tafiti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi katika kipindi cha miaka 60 iliyopita imehusishwa na maliasili.”

Katibu Mkuu amesema kutokana na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo yote , nafasi ya maliasili katika kuchochea mizozo itaongezeka sana. 

Tangu mwaka 1990, asilimia 75 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika kwa kiasi fulani vimefadhiliwa na mapato kutokana na maliasili. Uchimbaji haramu wa madini, ukataji wa mbao na magogo kinyume cha sheria pamoja na kusafirisha mkaa vimechochea ghasia.

Pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la idadi ya watu bado Katibu Mkuu amegusia suala la mgao usio sawia wa rasilimali hizo kwa wananchi akitaja chanzo ni rushwa na usimamizi mbaya ambao unaweza kusababisha mizozo hasa kwenye nchi zenye taasisi dhaifu.

Ametaja pia utoroshaji wa maliasili hizo na uchimbaji haramu wa rasilimali kama vile madini akitolea mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo amesema fedha zitokanazo na uchimbaji haramu wa rasilimali zimetumika kufadhili vikundi vilivyojihami.

“Tangu mwaka 1990, asilimia 75 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika kwa kiasi fulani vimefadhiliwa na mapato kutokana na maliasili. Uchimbaji haramu wa madini, ukataji wa mbao na magogo kinyume cha sheria pamoja na kusafirisha mkaa vimechochea ghasia,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu ametaka hatua zaidi zichukuliwe kusimamia uchimbaji, uuzaji na biashara ya madini taratibu za kiushirika zikihusisha vikundi vya kiraia, serikali na mashirika ya kitaifa na kimataifa.

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa unatambua nafasi ya ushirikiano wa mataifa katika kutumia vyema rasilimali asili ikiwemo maji kama njia mojawapo ya kuzuia mizozo na kuimarisha amani na usalama wa kikanda.

Amepigia chepuo mchakato wa Kimberley ambao amesema umesaidia kudhibiti biashara ya almasi pamoja na mipango ya pamoja ya matumizi bora ya maji ya bonde la mto Senegal.

Ametolea pia mfano wa Amerika ya Kusini, ambako bwawa la Titicaca, lililo kubwa kuliko yote barani Amerika limekuwa chanzo cha ushirikiano kati ya Bolivia na Peru.