Ajira milioni 24 kubuniwa duniani ifikapo 2030-ILO.
Ikiwa sera sawa za kukuza uchumi unaojali mazingira zitazingatiwa ifikapo mwaka wa 2030, ajira takriban milioni 24 zitabuniwa.
Kulingana na ripoti ya shirika la kazi duniani ILO, Ajira duniani pamoja na mwelekeo wa kijamii 2018, kujali mazingira na kazi iliyozinduliwa leo mjini Geneva, Uswisi ,hatua za kupunguza kiwango cha joto hadi nyuzi joto 2 katika kipimo cha selsiyasi, zitasababisha mazingira sawa ya kuunda ajira za kutosha ili kutoa pengo la ajira milioni 6 kwingineko.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Deborah Greenfield, amesema kuwa matokeo ya ripoti yao yanatilia mkazo kuwa ajira hutegemea mazingira mazuri ya kiafya na huduma zinazotolewa.
Ameongeza kuwa uchumi unaojali mazingira unawezesha watu mamilioni zaidi kuondokana na umaskini, na kuwa na maisha bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ripoti hiyo inasema kuwa ajira mpya zitabuniwa kwa kufuata mbinu endelevu katika sekta ya nishati ikiwemo mabadiliko kama vile kukuza matumizi ya magari yanayotumia umeme.
Bila kusahau mifumo ya huduma za ekolojia ikiwemo kusafisha hewa pamoja na maji, pembejeo, udhibiti wa wadudu waharibifu, kinga dhidi ya hali mbaya ya hali ya hewa pamoja na mengine mengi.
Pia uboreshaji wa sekta zingine kama uvuvi, kilimo, misitu na utalii ambavyo huajiri wafanyakazi bilioni 1.2, ikiwa utazingatiwa.
Hata hivyo ripoti hiyo kwa upande mwingine inapiga mahesabu kuwa msongo kutokana na joto, utasababisha hasara ya asilimia 2 katika saa za kazi ifikapo mwaka wa 2013 kutokana na watu kuugua.
Katika viwango vya kikanda bara la Asia litabuni ajira nyingi zaidi kuliko maeneo mengine kwani zitakuwa milioni 14, na kufuatiwa na eneo la Amerika litakalobuni ajira milioni 3 na lile la pasifiki na Ulaya kuchukua nafasi ya tatu kwa kiwango cha asilimia mbili.
Ripoti inaomba mataifa mengine yachukue hatua za kuwafundisha wafanyakazi mbinu mbadala zinazohitajika kuelekea uchumi usioharibu mazingira.