Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake bado watasalia nyuma katika soko la ajira duniani

Wafanyakazi wanawake wanaweka lebo kwenye saduku na mitungi kwa ajili ya usafirishaji na kuuzwa
FAO/Giulio Napolitano
Wafanyakazi wanawake wanaweka lebo kwenye saduku na mitungi kwa ajili ya usafirishaji na kuuzwa

Wanawake bado watasalia nyuma katika soko la ajira duniani

Wanawake

Licha ya mafanikio yaliyoshuhudiwa katika miaka 20 iliyopita , takwimu mpya za shirika la kazi duniani ILO zinaonyesha kuendelea kwa pengo la kutokuwepo usawa kati ya wanawake na wanaume katika soko la ajira, kutokuwa na kazi na mazingira ya kazi. 

Kwa mujibu wa matokeo ya ripoti ya utafiti mpya yaliyotolewa leo na ILO wanawake wana uwezekano mdogo wa kushiriki katika soko la ajira kuliko wanaume na wana uwezekano mkubwa wa kutokuwa na ajira katika sehemu nyingi duniani.

Ripoti hiyo “Mtazamo wa ajira na kijamii duniani :mwenendo wa wanawake kimataifa 2018” inasema mwaka huu  2018 ushiriki wa wanawake katika soko la ajira duniani ni asilimia 48.5, ambayo bado iko chini kwa asilimia 26.5 ukilinganisha na wanaume, huku kiwango cha kutokuwa na ajira kwa wanawake kikikwa asilimia 6.

Hii inmaanisha kwamba wakati kukiwa na wanaume 10 walio na ajira, upande wa wanawake ni 6 tu kote duniani. 

Deborah Greenfield ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa sera ILO amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na ahadi zilizotolewa ili kuboresha zaidi, matarajio ya wanawake katika ulimwengu wa kazi , bado kuna safari ndefu kuweza kuwa na usawa na wanaume.

Amesema iwe ni kuhusu upatikanaji wa ajira, pengo la mshahara au aina nyingine za ubaguzi, ulimwengu unahitaji kufanya kazi zaidi kubadilisha mwenendo huu usiokubalika kwa kuweka sera kwa ajili ya wanawake, pia kuzingatia majukumu makubwa yasio na usawa yanayowakabili katika kaya na utunzajiwa familia  na kwamba wanawake wengi walio katika ajira wako katika sekta isiyorasmi.

ILO inasema ili kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo basi pengo hilo kati ya wanawake na wanaume katika ajira ni lazima lizibwe. 

Utafiti huo uliangalia mambo manne, kwanza ushiriki katika soko la ajira, pili ukosefu wa ajira, tatu ajira zisizo rasmi na nne umasikini kazini.