Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumaliza vita ndio muarobaini wa njaa duniani

Wanawake huko Ganyiel jimbo la Unity nchini Sudan Kusini wakisubiri mgao wa chakula. Hali ni mbaya ya chakula.
OCHA/Gemma Connell
Wanawake huko Ganyiel jimbo la Unity nchini Sudan Kusini wakisubiri mgao wa chakula. Hali ni mbaya ya chakula.

Kumaliza vita ndio muarobaini wa njaa duniani

Msaada wa Kibinadamu

Mizozo na vita vinashika kasi kila uchao kwenye maeneo mbalimbali duniani. Katika mazingira hayo uzalishaji wa chakula ni tatizo, halikadhalika usafirishaji wa mazao ya chakula. Fedha nyingi hutumika kununua chakula cha msaada. 

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema amani na usalama duniani vitaepusha gharama kubwa inayotumika hivi sasa kukabiliana na baa la njaa na ukosefu wa chakula duniani.

Katika ripoti yake iliyotolewa mjini Roma, Italia hii leo, WFP imezingatia kuwa kadri baa la njaa na ukosefu wa chakula vinavyoenea duniani gharama kubwa ya fedha inatumika kununua chakula ili kupatia wahitaji.

Ripoti inasema kumaliza vita na mizozo ambavyo ni vichocheo vikubwa vya njaa, kunaweza kupunguza mahitaji ya msaada wa chakula kwa asilimia 50.

Kwa mantiki hiyo, ripoti hiyo ikinukuu vipimo vya Benki ya Dunia, inasema kuwa ongezeko la pointi moja tu ya amani na usalama duniani, linaweza kuokoa karibu dola bilioni 3 zinazotumika kununua chakula cha msaada.

Kuwepo kwa amani kunawezesha wakulima kama huyo pichani anayelima mihogo kuweza kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa chakula.
FAO/Giulio Napolitano
Kuwepo kwa amani kunawezesha wakulima kama huyo pichani anayelima mihogo kuweza kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa chakula.

Mathalani itaokoa dola milioni 3000 zinazotumika kwa ajili ya msaada wa chakula kwa wananchi wa Syria, na dola milioni 205 kwa wananchi wa Yemen.

Mkuu wa WFP anayehusika na mifumo ya chakula, Steven Were Omamo ambaye ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo amesema kuzuia janga la chakula kunahitaji pia uwekezaji wa muda merfu kwenye elimu, miundombinu na ukuaji wa uchumi.

Amesema kwa kuzingatia hayo, matumizi ya WFP kwenye misaada ya chakula yatapngua kwa dola bilioni 5 na hatimaye fedha hizo zitaelekezwa kwenye matumizi mengine ya kuboresha maisha ya walio hatarini zaidi.