Uboreshaji makazi Korea Kusini waengua maskini

11 Mei 2018

Nchini Korea Kusini suala la uboreshaji wa makazi duni limekuwa na madhara makubwa kwa watu wa kipato cha chini.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa atazuru Korea Kusini kuanzia wiki ijayo kuangazia suala la haki ya makazi kwa wananchi.

Ziara hiyo inafuatia ripoti  ya kwamba wananchi wa kawaida wanashindwa kumudu makazi yenye hadhi wakati huu ambapo sera za kuboresha maeneo ya makazi duni zinaengua wakazi maskini pindi uboreshaji wa maeneo hayo unapokamili.

Mtaalamu huyo Leilani Farha ambaye anahusika na haki ya makazi amesema wakati wa ziara hiyo ya siku 10 atachunguza iwpao mazingira ya nyumba kwa makundi yaliyo hatarini zaidi  yanazingatia viwango vya haki za binadamu vya kimataifa.

Amesema licha ya kuwepo kwa ripoti za uboreshaji wa makazi, bado upatikanaji wa nyumba na ongezeko la watu wasio na makazi vinatiwa wasiwasi mkubwa.

Mathalani amesema sera za uboreshaji wa makazi duni zimekuwa na athari mbaya kwa jamii zilizo hatarini zaidi ikiwemo vijana wanaosaka nyumba kwa kuwa hawawezi kuzimudu.

Kama hiyo haitoshi, wazee nao ambao wanahaha kubakia kwenye maeneo hayo wanakumbwa na sintofahamu kwasababu gharama zinakuwa ni za juu na hawawezi kuendelea kuishi kwenye makazi hayo.

Kwa mantiki hiyo Bi. Farha atajadili na mamlaka sababu na athari za uwekezaji kwenye makazi na kuangalia njia mpya za kupanua wigo ili uwekezaji huo usikwapue haki za binadamu za wananchi maskini.

Ziara yake inafuatia mwaliko wa serikali ya Korea Kusini ambapo akiwa nchini humo atakuwa na mazungumzo na viongozi wa serikali, wasomi, na vikundi vya kiraia.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter