Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera mpya ya makazi nchini Canada ni mfano kwa nchi nyingine-Mtaalamu wa UN

Jengo ndefu la mbao. (picha ya maktaba)
Naturallywood.com / KK Law
Jengo ndefu la mbao. (picha ya maktaba)

Sera mpya ya makazi nchini Canada ni mfano kwa nchi nyingine-Mtaalamu wa UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi,  Bi. Leilani Farha akiwa mjini Geneva, Uswisi  hii leo anasema serikali ya Canada imeweka mfano duniani  kwa sera yake mpya ya makazi ambayo inahusisha haki za binadamu kama mfumo bora zaidi wa kushughulikia kutokuwepo kwa makazi na pia makazi duni.

Bi Farha amesema, “tukiwa na miaka 10 kabla ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs, serikali ya Canada imebadili namna yake ya kutekeleza haki ya makazi kuwa ile inayotambua makazi kama haki msingi ya binadamu na iliyo ya muhimu kwa ustawi na utu wa mtu. Mfano mpya wa Canada una sifa za haki za binadamu. Siyo tu inajumuisha sheria iliyo na haki ya kumiliki nyumba, pia unaanzisha mfumo wa ubunifu wa sheria kuifuatilia Serikali kuwajibika na kuhakikisha upatikanaji wa tiba za kukabiliana na vikwazo vya utaratibu wa kufurahia makazi bora. Mfano huu unaweza kutumika kama mfano kwa nchi zote duniani kote.”

Farha amesema pamoja na Canada kuwa katika nafasi ya 10 duniani  kiuchumi, kuna watu takribani 235,000 wasio na makazi na kaya milioni 1.34 zenye uhitaji wa makazi katika miji kadhaa.

Imeelezwa kuwa Canada hivi karibuni itateua mchechemzi wa kujitegemea wa makazi ambaye atakuwa anafuatilia utendaji wa serikali, kufuatilia maoni kuhusu vikwazo vya kuwa na nyumba za kutosha, ikiwemo na matumizi ya bajeti na kufanya majadiliano mbele ya jopo la wazi kupitia masuala kadhaa ambayo bunge lina mamlaka nayo. Matokeo na ushauri vitakabidhiwa kwa waziri anayehusika ambaye atawasilisha kwa bunge.

“Kwa sasa kuna watu bilioni 1.8 duniani kote ambao wanaishi katika mazingira ya kukosa makazi na wanaoishi katika makazi duni. Ninazisihi nchi zote kutekeleza haki ya makazi kwa nguvu zote kupitia mikakati hii ya kuwa makazi ni haki na ni njia pekee ambapo janga la dunia la ukosekanaji wa makazi litaweza kutatuliwa kufikia mwaka 2030.” Amesisitiza Bi Farha.