Mataifa yanawaangusha mamilioni ya watu wasio na makazi-Mtaalamu wa UN

4 Machi 2019

Mataifa hayawezi kujipambanua kama viongozi wa haki za binadamu ilihali wakiacha idadi inayoongezeka ya watu wasio na makazi wakiishi na kufa katika mitaa yao bila namna ya kuziwajibisha serikali zao, ameeleza leo mjini Geneva, Uswisi Leilani Farha mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki ya makazi.

Tovuti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifaifa (OHCHR) imemnukuu Leilani Farha akisema, “wakati wa visingizio, uhalalishaji na kutoa kisogo wakati haki ya makazi inapominywa umepitwa . Haki zinapaswa kuwa na tiba na serikali zinatakiwa kuwajibika kwa wenye haki.”

Mtaalamu huyo ameeleza pia kuwa uhamishaji wa wale wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi pasipo kufuata maagizo ya mahakama na utawala wa kisheria vinamaanisha kuwa wale ambao haki yao ya makazi imekiukwa wamekuwa hawatambuliwi na hawatendewi kama binadamu wengine.

Katika ripoti yake, Farha anasema kuwa mgogoro wa ukosefu wa makazi duniani umejikita katika ukosefu wa wa mazingira ya kupata haki kisheria kwasababu bila haki hiyo, makazi hayatambuliwi au kueleweka ipasavyo na pia kushughulikiwa kama haki ya binadamu.

“Mamilioni ya wanaoishi bila makazi au katika makazi duni, hawana mahali ambako wanaweza kudai haki yao ya makazi wakati ambapo mataifa yameshindwa kutambua haki, kuwahamisha kwa nguvu au kuwaona wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi kuwa ni wenye makosa” amesisitiza mtaalamu huyo.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter