Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake ndio wanaobeba gharama kubwa ya huduma zisizo na ujira:ILO

Kuna zaidi ya wanawake milioni 11 duniani kote ambao wanatumikishwa bila vibali.
ILO
Kuna zaidi ya wanawake milioni 11 duniani kote ambao wanatumikishwa bila vibali.

Wanawake ndio wanaobeba gharama kubwa ya huduma zisizo na ujira:ILO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Uwekezaji katika uchumi utokanao na sekta ya huduma unahitaji kupigwa jeki mara mbili ili kuepuka janga la kimataifa linalonyemelea katika sekta hiyo, imesema ripoti mpya ya shirika la kazi duniani ILO iliyotolewa leo

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iitwayo” “kazi na ajira za utoaji huduma kwa ajili ya mustakhbali wa ajira zenye hadhi” inaonyesha kwamba wanawake wanatumia robo tatu zaidi ya muda wao katika kazi za kutoa huduma zisizo na ujira ikilinganishwa na wanaume na wanawake wengi ndio wanaofanya kazi za malipo za utoaji huduma. Shauna Olney ni mkuu wa kitengo cha jinsia, usawa na utofauti katika idara ya msaada ya ILO anasema

SAUTI YA SHAUNA OLNEY

“Huduma ni suala mtambuka kwa kuwafanya wanawake wawe nje ya kazi, kwa kuwazuia wasiendelee katika ulimwengu wa ajira na kudumu katika kazi, hivyo kushughulikia suala la huduma za malipo na zisizo za malipo ni muhimu kama kweli tunataka kufikia malengo ya usawa wa kijinsia, kama tunataka kuepuka janga katika sekta ya huduma na kama kweli tunajali mustakhbali wa ajira”

 Ripoti imebaini kuwa kote duniani ajira mpya milioni 269 zinaweza kuundwa endapo uwekezaji utaongezwa mara mbili katika elimu, afya na kazi za kijamii ifikapo mwaka 2030.

Pia imetaka mabadiliko makubwa katika será yashughulikie ongezeko la mahitaji ya huduma na pengo kubwa lililopo baina ya wanawake na wanaume katika majukumu ya kutoa huduma. Shauna Olney anaongeza

SAUTI YA SHAUNA OLNEY -2

“Inakadiriwa kwa mwaka 2018 saa bilioni 16.4 zitatumika kwa kazi za huduma zisizo na malipo kila siku, sawa na watu bilioni 12 wanaofanya kazi kwa saa 8 bila ujira kila siku. Kote duniani wanawake wanafanya asilimia 76.2 ya jumla ya saa zote za kazi za bila malipo ikiwa ni mara tatu zaidi ya wanaume.”

Ripoti hiyo ambayo imependekeza hatua mbalimbali ikiwemo kuziba pengo la usawa katika ajira za malipo na zisizo na malipo, imetokana na takwimu zilizokusanywa kutoka nchi 64 zinazowakilisha theluthi mbili ya watu wote duniani walio na umri wa kufanya kazi , na imebainisha kwamba watu zaidi ya bilioni 2 walihitaji huduma mwaka 2015 wakiwemo watoto wa chini ya umri wa miaka 15 wapatao bilioni 1.9 na wazee milioni 200, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia bilioni 2.3 mwaka 2030.