Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 2 kupatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu Afrika

Harakati za chanjo dhidi ya kipindupindu. (Picha:UN/Logan Abassi)

Watu milioni 2 kupatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu Afrika

Afya

Kampeni kubwa ya aina yake ya chanjo dhidi ya kipindupindu inafanyika kwenye nchi tano barani Afrika ili kudhibiti mlipuko wa gonjwa hilo.

Nchi hizo ni Nigeria, Zambia, Malawi, Uganda, Sudan Kusini na Malawi ambapo walengwa kwenye nchi hizo ni watu milioni mbili.

Ubia wa chanjo duniani, GAVI ndio umewezesha kupatikana kwa chanjo hizo ambapo kila mlengwa atapatiwa dozi mbili, kampeni ikitekelezwa kwa ushirikiano na wizara za afya za nchi husika.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linasema dozi ya kwanza ni ya kinga kwa miezi 6 ilhali ya pili inatoa kinga ya kati ya miaka mitatu hadi mitano.

Akizungumzia kampeni hiyo, Dkt. Seth Berkely ambaye ni afisa mtendaji mkuu wa GAVI amesema ingawa wanatoa chanjo, vado kuna umuhimu wa kuboresha huduma za kujisafi kwa kuwa ndio suluhu ya kudumu ya kukabiliana na milipuko ya kipindupindu.

Awamu ya pili ya dozi hizo inatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi ujao.

Ugonjwa wa kipindupindu umesalia mzigo kwa nchi nyingi za Afrika ambapo hata hivyo matumizi ya chanjo dhidi  ya ugonjwa huo yameleta matumaini makubwa.