Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita dhidi ya malaria imeenda kombo tuirejeshe mstarini: WHO

Kampeni ya kutokomeza malaria kwa kufundisha wananchi matumizi na umuhimu wa vyandarua vyenye dawa nchini Tanzania. Picha na WHO

Vita dhidi ya malaria imeenda kombo tuirejeshe mstarini: WHO

Afya

Kwa mara ya kwanza katika muongo mmoja uliopita hatua za kuelekea kutokomeza malaria zimekwaa kisiki na mafanikio yaliyopatikana yakishuhudiwa kubadili mwelekeo katika baadhi ya nchi kote duniani.

Kwa mara ya kwanza katika muongo mmoja uliopita hatua za kuelekea kutokomeza malaria zimekwaa kisiki na mafanikio yaliyopatikana yakishuhudiwa kubadili mwelekeo katika baadhi ya nchi kote duniani.

Hayo yamesemwa na shirika la afya ulimwenguni WHO hii leo ikiadhimishwa siku ya malaria duniani, na kuongeza kuwa mwaka 2016 umekuwa na visa milioni 216 huku vifo 445,000 vikiripotiwa kutokana na ugonjwa huo hatari.

Akizungumza mjini Geneva Uswisi Pedro Alonso, mkurugenzi wa mpango wa kimataifa wa malaria amesema kauli mbiu ya siku yamalaria mwaka huu ni kuwa “Tayari kuitokomeza malaria” kwani kwa sasa dunia imefikia ukomo wa nini itakachoweza kufanikiwa kwa rasilimali chache iliyonazo hivyo amesisitiza kuwa mafanikio ya vita dhidi ya malaria yanahitaji

(Sauti ya Pedro Alonzo)

“Kufufua utashi wa kisiasa, kuongeza rasilimali fedha kutoka kwa nchi wahisani na nchi zilizoathirika na malaria, na pia nyenzo mpya na zilizoboreshwa za kupima na kutibu malaria.”

Lengo kuu likiwa kuzisaidia nchi zinazobeba mzigo mkubwa wa gonjwa la malaria ambazo nyingi ziko Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.

Dkt.. Matshidiso Moeti ni mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika bara linalobeba asilimia 90 ya mzigo wa malaria na asilimia 91 ya vifo vyote vya gonjwa hilo.

(Sauti ya Dkt. Matshidiso Moeti)

“Sisi kama ukanda wa Afrika, viongozi wetu wa kitaifa na serikali zetu lazima zichukue hatua za makusudi kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya lakini pia watambue kuwa kinga dhidi ya Malaria  na tiba ni uwekezaji mzuri.”

WHO imetoa wito wa hatua za haraka kurejesha vita vya kimataifa dhidi ya malaria katika msitari unaotakiwa baada ya kwenda kombo, ili kufikia lengo namba 3.3 la SDGs la kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.