Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya Ebola yaanza kutolewa nchini Cote d’Ivoire

Watoa huduma wa afya wakipokea chanjo ya Eboja mjini Abidjan, Cote d'Ivoire
WHO
Watoa huduma wa afya wakipokea chanjo ya Eboja mjini Abidjan, Cote d'Ivoire

Chanjo ya Ebola yaanza kutolewa nchini Cote d’Ivoire

Afya
  • Watoa huduma na waliokuwa karibu na mgonjwa waanza kupata chanjo
  • Mtu mwingine anahisiwa kuwa na dalilia za Ebola
  • WHO yapongeza utoaji chanjo haraka na ushirikiano wanchi

Watoa huduma nchini Cote d’lvoire wameanza kupatiwa chanjo ya Ebola ikiwa ni siku chache ( 14 Agost 2021) tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO litangazwe uwepo wa ugonjwa huo nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na WHO imesema uchomaji chanjo ya Ebola ya rVSV-ZEBOV umeanza rasmi 16 Agosti 2021 mjini Abijan, baada ya WHO kuisaidia Cote D’Ivore kupata chanjo kutoka nchi jirani ya Guinea ambayo kwa miezi minne ilikuwa ikipambana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Tangu mlipuko wa Ebola utangazwe nchini Guinea mwanzoni mwa mwaka huu 2021, WHO imekuwa ikizisaidia nchi 6 za Jirani ikiwemo Cote d’lvoire kujiandaa na mlipuko wa ugonjwa huo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo timu kujipanga kwa haraka kukabiliana nao, vifaa vya kupimia, uwezo wa kuwapatia matibabu, utoaji elimu kwa um ana ushirikiano.

Akipongeza hatua hiyo ya haraka ya utoaji chanjo mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO ,Dkt. Matshidiso Moeti, amesema "Kasi ambayo Cote d'Ivoire imeonyesha kwenye utoaji chanjo ni ya kushangaza na inaonyesha kuwa kwa mshikamano mzuri wa kikanda tunaweza kuchukua hatua za kuzima maambukizo mabaya ambayo yanaweza kutokea hadi milipuko mikubwa."

Cote d'Ivoire imezindua kampeni ya utoaji chanjo ya Ebola kwa watoa huduma walio mstari wa mbele
WHO
Cote d'Ivoire imezindua kampeni ya utoaji chanjo ya Ebola kwa watoa huduma walio mstari wa mbele


 Utoaji Chanjo

“Chanjo ya Ebola ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya virusi, hivyo ni kipaumbele chetu cha juu kabisa ili kusonga mbele kwa kasi na kuanza kulinda watu walio katika hatari kubwa yakupata maambukizi ya ugonjwa huo." Amesema Dkt.Moeti

Pamoja na mtu mmoja aliyethibikita kuugua Ebola, uchunguzi unaoendelea umebaini mtu mmoja kuhisiwa kuwa na Ebola pamoja watu wengine tisa ambao walikutana naye kuendelea kuwekwa kwenye uangalizi. Hakuna kifo kilicho ripotiwa. 

Wataalamu watano wa chanjo kutoka Guinea wamewasilini nchini Cote d’Ivore kwa ajili ya kutoa chanjo kwa mgonjwa wa Ebola. 
Utoaji chanjo kutoka nchini Guinea umejumlisha dozi 200 kutoka Merck ambazo wanapewa watu ambao wamekutana na mgonjwa aliyethibitishwa wa Ebola, pamoja na watoa huduma wa sekta ya afya.

Guinea pia imetuma chanjo 3000 za kampuni ya Johnson & Johnson ambazo zitatumika kuwapatia watu walio kwenye maeneo yenye maambukizi yanayoendelea. 

Mpaka sasa hakuna dalili zinazoonesha mlipuko wa sasa huko Cote d'Ivoire unahusishwa na ule uliokuwa nchini Guinea. Uchunguzi zaidi unaendelea kubaini iwapo kuna uhusiano wowote.

Cote d’lvoire ni nchi ya tatu kupata mlipuko wa Ebola kwa mwaka huu baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC na Guinea.