Ghasia Nicaragua zikome- Guterres

17 Julai 2018

Wakati idadi ya watu waliouawa nchini Nicaragua tangu maandamano dhidi ya serikali yaanze nchini humo ikiwa ni takribani 280, Umoja wa Mataifa umesema ni dhahiri shahiri kuwa lazima ghasia hizo zikome hivi sasa.

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa huo, Antonio Guterres akizungumza akiwa ziarani Costa Rica amesema kukoma kwa ghasia ni muhimu ili mashauriano ya kisiasa yaweze kuanza kwa kuwa suluhu ya kisiasa ndio muarobaini wa kinachoendelea nchini humo.

 (Sauti ya Antonio Guterres)

 “Ghasia hazitaruhusu suluhu kupatikana kwa hiyo ni muhimu kurejelea ripoti ya tume ya haki za binadamu ya nchi za Amerika na hatua za ofisi ya haki za binadamu, pamoja na kuhakikisha serikali inawajibika kulinda raia. Wajibu huu wa msingi hauwezi kusahaulika hasa wakati huu ambapo kuna idadi kubwa ya kushtusha ya watu waliopoteza maisha..”

Nayo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetaka ghasia hizo zikoke hivi sasa ikiongeza kuwa ni vyema serikali ambayo inajiwabika kwa sheria za kimataifa itoe hakikisho la haki ya uhai na ulinzi kwa watu wote pamoja na uhuru wa kujieleza na kuandamana.

Artículo 66
Mabango mjini Masnagua katika maandamano ya kudai kukomesha machafuko nchini Nicaragua

Katibu Mkuu alipoulizwa na waandishi wa habari ni hatua gani Umoja wa Mataifa unachukua amesema kuwa..

“Mimi ni mtetezi wa hoja ya kwamba matatizo ya nchi yanatatuliwa vyema pindi ukanda husika unapobeba jukumu la kuongoza harakati za kimataifa za kusaka suluhu. Sisi tupo kusaidia juhudi za SICA kama vile ushirika wa nchi za Amerika. Kwa upande mwingine, tayari tumetuma ujumbe kutoka idara ya siasa ya Umoja wa Mataifa na kamishna wa haki za binadamu naye ametoa taarifa zake.”

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville amesema..

“Hali inakuwa mbaya zaidi kwa kuwa vikundi vilivyojihami ambavyo vinaunga mkono serikali vinatekeleza operesheni zao kwa kisiri huku vikiungwa mkono na polisi na  mamlaka za serikali.”

Ameongeza kuwa wakati huu ambapo kuna ongezeko la mazingira ya hofu na kutokuaminia,  kuna hofu ya kuongezeka kwa ghasia kwa kuwa Nicaragua inajiandaa kuadhimisha siku ya ukombozi tarehe keshokutwa Ijumaa, ikiwa ni kumbukizi ya kuondolewa madarakani kwa utawala wa Somoza mwaka 1979.

Maandamano yameanza takribani miezi mitatu iliyopita ambapo waandamanaji wanataka kuondoka madarakani kwa Rais Daniel Ortega.

Hadi sasa watu wapatao 280 wameuawa na wengine zaidi ya 1800 wamejeruhiwa, watetezi wa haki za binadamu nao wanashambuliwa huku wengine wakiwa wametoweshwa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud