Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bodaboda nayo yaweza imarisha amani Sudan Kusini

Mamia ya waendesha bodaboda huko Juba, baada ya mafunzo ya usalama barabarani yaliyoendeshwa na UNMISS Sudan Kusini.Katika maeneo mengi duniani kazi hii ya uendeshaji bodaboda imekuwa ikionekana kuwa ni kazi ya kiume.
UN/Isaac Billy
Mamia ya waendesha bodaboda huko Juba, baada ya mafunzo ya usalama barabarani yaliyoendeshwa na UNMISS Sudan Kusini.Katika maeneo mengi duniani kazi hii ya uendeshaji bodaboda imekuwa ikionekana kuwa ni kazi ya kiume.

Bodaboda nayo yaweza imarisha amani Sudan Kusini

Amani na Usalama

Amani na Usalama ni mambo yanayoenda pamoja na ndivyo hivyo ambavyo Umoja wa Mataifa umetumia mbinu mpya ya kuwajumuisha waendesha bodaboda huko Sudan Kusini ili wawe sehemu ya kuchagiza na kueneza amani kwenye nchi hiyo ambayo tangu disemba 2013 vuta nikuvute imeshamiri.

Kuelekea wiki ya usalama barabarani duniani huko Sudan Kusini Umoja wa Mataifa umezindua kampeni yake inayolenga kuimarisha amani na usalama kupitia usafirishaji wa abiria kwa kutumia bodaboda. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, waendesha bodaboda wakivinjari bila kofia za kuhakikisha usalama wao.

Ingawa hivyo msafara huu ni wa kuelekea kupatiwa vifaa hivyo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutumia bodaboda kuchagiza amani na usalama.

Katika kituo cha polisi, wanapatiwa vizibau vyenye rangi ya kuangaza iwe usiku au mchana, kwa lengo la kuweza kutambuliwa, halikadhalika kofia ngumu za kuvaa waendeshapo bodaboda.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umechukua hatua hii ikilenga takribani waendesha bodaboda 3,000 wanaosafirisha abiria mchana na usiku mjini Juba.

Wakati kampeni ya amani na usalama kupitia bodaboda ikizinduliwa Juba, Sudan Kusini, wachuuzi wa maembe na ndizi nao walitumia fursa kujipatia kipato.
UN/Isaac Billy
Wakati kampeni ya amani na usalama kupitia bodaboda ikizinduliwa Juba, Sudan Kusini, wachuuzi wa maembe na ndizi nao walitumia fursa kujipatia kipato.

Kupitia kampeni ya endesha kwa amani na usalama inayofanywa kwa ubia kati ya UNMISS na chama cha wamiliki wa Bodaboda Sudan Kusini, waendesha bodaboda wanapata fursa pia ya kufahamu shughuli za ujumbe huo.

(Sauti ya Morbe Andrew)

 “Nchini Sudan Kusini, vijana wamekuwa wakitumiwa ambako hawapati amani. Kwa hiyo kama kijana tunavyoendesha kwa amani hii leo, utaona amani itakuwepo Sudan Kusini.”

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini David Shearer ambaye pia ni mkuu wa UNMISS akafunguka…

(Sauti ya David Shearer)

 “Ni kuhusu ulinzi na tunalinda raia kwenye mizozo lakini pia mitaani. Iwapo tunaweza kufanya watu wajihisi salama wanapopanda bodaboda asi itakuwa vyema kwa kila mtu.”

Na ndipo naye Bwana Shearer alivaa kizibau na kofia na kukwea bodaboda ili kupata uzoefu halisi.