Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna haja ya kujikita na waathirika wakubwa wa mzozo wa Sudan Kusini:UN/AU

Baadhi ya waathirika wa mgogoro wa Sudan Kusini
UNMISS/Isaac Billy
Baadhi ya waathirika wa mgogoro wa Sudan Kusini

Kuna haja ya kujikita na waathirika wakubwa wa mzozo wa Sudan Kusini:UN/AU

Amani na Usalama

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU ambao uko ziarani Sudan Kusini kwa siku tatu, umeonyesha mshikamano wake na watu pamoja na uongozi wa nchi hiyo ukisema uko tayari  kuunga mkono mkataba wa amani uliotiwa saini hivi karibuni mjini Addis Ababa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  leo mjini Juba na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo UNMISS pia ziara hii inalenga  kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake na wasichana nchini humo.

Wakizungumza baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juba, mkuu wa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix na  Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka, wamesema kuna haja ya kuwashughulikia zaidi wale ambao ni waathirika wakubwa wa vita, wanawake na watoto.

Maendeleo ya Sudan Kusini yamedumazwa na mgogoro  ambao umeendelea kwa miaka zaidi ya mitano sasa, hata hivyo kuna matumaini kuwa mkataba wa amani uliotiwa sahihi Septemba 12 nchini Ethiopia,utakomesha ghasia ambazo zimesababisha watu zaidi ya milioni nne kubaki bila makazi.

Bw Lacroix, amesema “ tuko katika wakati ambao mkazo ni lazima uwekwe kwenye utekelezaji wa mkabta za amani uliopitishwa, tuko tayari kusaidia, na tuko tayari kuunga mkono, na kwa wakati huu tuko tayari kusema kuwa ni muhimu kutafakari mahitaji ya kutekeleza mkataba ambayo ni ujumuishwaji.”

Kuhusu haki za wanawake ambao ni waathirika wakubwa wa mgogoro huo Lacroix amefunguka“ sauti za wanawake zikisikika, hii inadhirisha kuwa wanawakilishwa katika  mchakato wa kuleta amani nchininSudan Kusini. Ingawa kuna nuru inakuja lakini tunafahamu kuwa mengi yanahitajika kufanyika na nasi tuko hapa tutasaidia. Na njia pekee ya kuleta amani ya kudumu ni kujenga amani jumuishi.”

Naye Phumzile Mlambo-Ngcuka mkuu wa UN-Women, amesema lengo la ziara yao hii ni kumulika wanawake, amani na usalama kwa sababu ya athari ya mgogoro huo kwa wanawake.

“Tunataka kuhakikisha kuwa mazungumzo yote yanayoendelea ni sharti yawahusishe wanawake katika njia inayofaa. Wanawake wanahitaji kuungwa mkono na kulindwa lakini wanawake ni baadhi ya walio na uamuzi, na mkataba wa manai wa mwezi septemba  una nafasi asilimia 35 za uongozi ambazo zilitengwa kwa ajili ya wanawake pekee, ni hatua nzuri na tungependa mengi zaidi yafanywe.”

Mjumbe kutoka Muungano wa Afrika, Dkt Specioza Wandira -Kazibwe, ambae pia ni mwenyekiti wa asasi ya Mtandao wa wanawake wa Afrika unaoshughulika na ppatanishi- FemWise, amesema kuwa anataka kuwahimiza wanawake nchini Sudan Kusini kuungana na wanaume katika mapambano ya kuendeleza nchi yao.