Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufilipino nayo yafuata nyayo kujiengua ICC

Jengo la ICC. (Picha@ICC)

Ufilipino nayo yafuata nyayo kujiengua ICC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Serikali ya Ufilipino imeomba kujiondoa kutoka mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC baada ya kuridhia mkataba wa mahakama hiyo Agosti 2011.

Febuari 2018 ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ilitangaza kuanza mchakato wa uchunguzi   wa makosa ya jinai yanayodaiwa kufanywa na vikosi vya serikali ya Ufilipino katika vita ilivyotangaza  dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya  vilivyoanza Julai mosi 2016. Kuna madai kuwa makosa ya jinai mengi yamefanywa na vikosi vya usalama wakati vikitekeleza operesheni hiyo.

Umoja wa Mataifa unasema  Machi 19, 2018  umeifahamisha rasmi mahakama ya ICC kuhusu ombi la Ufilipino kutaka kujiondoa. Machi 17, 2018 serikali ya Ufilipino , iliwasilisha hati rasmi ya kutaka kujiondoa kutoka mkataba wa Roma uliozaa mahakama ya ICC. Kikanuni katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huwa ndiye mlezi wa mkataba huo.

Taarifa kutoka ICC inasema kuwa mahakama hiyo inasikitishwa   na tukio hili na  kuitaka  Ufilipino kufikiria upya ili kubaki kama sehemu ya familia ya ICC.

Kwa mujibu wa mkataba wa ICC, uamuzi wa kujiondoa ni wa hiari japo hatua inatakiwa ifuate   kifungu 127 cha sheria . ICC imeeleza kuwa  rasmi mtu hujiengua mwaka mmoja baada ya kuwasalisha maombi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kujiondoa huko hakuathiri uchunguzi ambao unaendelea au jambo lolote ambalo limeamuliwa na mahakam hiyo kulishughulikia kabla ya tarehe ya kujiondoa kufika.