ICC yachunguza Venezuela na Ufilipino

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) Fatou Bensouda.(Picha:UM/Manuel Elias)

ICC yachunguza Venezuela na Ufilipino

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, Fatou Bensouda ameamua kuanzisha uchunguzi wa awali dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa kile kilichopatiwa jina la operesheni maalum nchini  Venezuela na Ufilipino.

Akizugnumza hii leo huko The Hague, Uholanzi Bi. Bensouda amefafanua sababu za kuchukua hatua hiyo dhidi ya Ufilipino.

(Sauti ya Fatou Bensouda)

Tangu julai Mosi mwaka 2016 Ufilipino ilianzisha operesheni maalumu dhidi ya kile ilichokiita vita dhidi ya madawa ya kulevya . Inadaiwa kuwa tangu tarehe hiyo maelfu kadhaa ya watu wameuawa kwa sababu zinazohusika na madai ya kujihusisha katika matumizi ya madawa haramu au ulanguzi wa madawa yenyewe.

Bi. Bensouda amesema ni katika harakati hizo watu waliuawa na visa vingine vya mauaji vikidaiwa kufanywa na vikosi vya ulinzi na usalama.

Kuhusu Venezuela mwendesha mashtaka huyo mkuu wa ICC anasema kuwa uchungunzi utajikita katika makosa yanayodaiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka 2017 katika muktadha wa maandamano na vurugu zilizofuatia..

(Sauti ya Fatou Bensouda)

 “Inadaiwa kuwa  vikosi vya usalama vya taifa kila mara vilikuwa vikitumia nguvu kupita kiasi wakati wa kuzima maandamano hayo au kuyasambaratisha. Wakati huo vikosi hivyo viliwakamata na kuwatia kuzuizini maelfu ya watu ambao baadhi ni wanachama wa upande wa upinzani ilhali wengine walidhaniwa kuwa hivyo”.

Hata hivyo amesema katika visa hivyo baadhi ya waandamanaji walitumia fujo na kusababisha  wana usalama kujeruhiwa au kuuawa.