Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufutiwa viza ya Marekani hakumzuii Bensouda kuendelea na majukumu yake- ICC

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya  ICC
UN Photo/Rick Bajornas)
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC

Kufutiwa viza ya Marekani hakumzuii Bensouda kuendelea na majukumu yake- ICC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC, imethibitisha kuwa serikali ya Marekani imefuta kibali cha kuingia nchini humo cha mwendesha mashtaka mkuu huyo Fatou Bensouda.

Hata hivyo ofisi hiyo imesema hatua hiyo katu haitamzuia yeye na wafanyakazi wenzake kuendelea kutekeleza majukumu yao.

Bi. Bensouda anakuwa muathirika wa kwanza wa uamuzi wa Marekani kufuta kibali cha kuingia nchini humo kwa wafanyakazi wa ICC ambao wanachunguza harakati za jeshi la Marekani nchini Afghanistan.

Mwenzu Novemba mwaka 2017, Bi. Bensouda aliomba kibali kutoka mahakama ya ICC ili aanze uchunguzi wa uhalifu dhidi ya kibinadamu uliotekelweza nchini Afghanistan tangu mwezi Mei mwaka 2003, akisema kuwa anaamni kuwa misingi ya kutosha ya kuthibitisha kuwa wakati wa vita vya Afghanistan, jeshi la Marekani lilitekeleza uhalifu wa kivita. Hata hivyo hadi sasa hata hivyo majaji bado hawajatoa uamuzi wa kukubali kufanyika uchunguzi huo au la.

Mwezi Machi mwaka huu, Waziri wa Mambo  ya Nje wa Marekani Michael Pompeo alitangaza kuwa serikali yao haitawapatia vibali vya kuingia nchini Marekani wafanyakazi wa ICC na itafuta vibali ambavyo tayari vimetolewa kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo yenye makao yake makuu huko The Hague, Uholanzi.

Taarifa ya Ofisi ya mwendesha mashtaka iliyotolewa leo hata hivyo inasema, “kuna uelewa kuwa uamuzi huo wa kumnyima kibali hicho au Viza, hautakwamisha harakati za Bi. Bensouda ikiwemo kufika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, na kuhutubia vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”

Halikadhalika taarifa hiyo imesema kuwa ofisi hiyo ya mwendesha mashtaka wa ICC ni huru na haiegemei upande wowote kwa mujibu wa mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo na kwamba itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa azma ya juu ya ueledi bila woga wa upendeleo.