Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna alama za mauaji ya kimbari Myanmar-UN

Yanghee Lee, mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Myanmar
Picha na UN/Kim Haughton
Yanghee Lee, mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Myanmar

Kuna alama za mauaji ya kimbari Myanmar-UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuna dalili za mauaji ya kimbari katika mkoa wa Rakhine dhidi ya warohingya.Hayo yametamkwa  na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu  nchini Mynamar, Yanghee Lee, wakati akilihurubia baraza la haki za binadamu jumatatu mjini Geneva

Akifafanua hilo amesema kuwa kwa maoni  yake anahisi kuwa matukio katika mkoa wa Rakhine, unaopatikana nchini Myanmar,  yana alama za mauaji ya kimbari na kutaka kuwepo uwajibishwaji.

Mwaka jana Lee alizuiliwa  kuingia nchini Myanmar, na leo jumatatu ametoa wasiwasi wake  kuwa huenda vitendo vya ukandamizaji vya serikali za kijeshi zilizopita  ndio vinarejea nchini Myanmar, akieleza kama hali inayoyakabili makundi ya kiraia nchini humo ni ya kuhatarisha.

Lee ametaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa haraka bila kuchelewa  na wahusika  wachukuliwe hatua dhidi ya  makosa yanayodaiwa kufanyika  katika mkoa wa Rakhine kuanzia tarehe  Oktoba mwaka 2016  na Agosti 25 mwaka 2017, pamoja na fujo zinazoendelea hadi sasa.

Ameongeza kuwa dunia sasa imejikita na   mgogoro  wa mkoa wa Rakhine na kupuuza ghasia katika mikoa ya Kachim, Shan na pia mikoa mingine nchini Myanmar ambayo imeathirika na machafuko kama hayo.