Myanmar ipelekwe ICC- Zeid

4 Julai 2018

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein amelisihi Baraza la Usalama la umoja huo liipeleke Myanmar kwenye mahakama ya kimataifa ya  uhalifu, ICC.

Zeid amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati akihutubia Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa baada ya kuwasilisha ripoti yake kuhusu kinachoendelea nchini humo.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia vitendo vya ukatili vinavyoendelea dhidi ya waislamu wa kabila la rohingya na kwamba hadi sasa Myanmar haijatekeleza ahadi yake ya kuruhusu warejee nyumbani.

«Mamlaka za Myanmar zimekuwa zikihoji madai ya kwamba majeshi yake yanatekelea mauaji ya kikabila yaliyochochoea zaidi ya warohingya 700,000 wakimbilie Bangladesh tangu Agosti mwaka jana. Mamlaka hizo pia zimeendelea kutumia nguvu nyingi kujaribu kushawishi dunia kuwa iko tayari kuruhusu wakimbizi warejee, » amesema Bwana Zeid.

Amesema hadi sasa hakuna kinachoendelea zaidi ya wahoringya kuendelea kumiminika Bangladesh huku wakilalama juu ya mateso na ukatili dhidi yao kutoka mikononi mwa jeshi la Myanmar.

Wanawake wawili wakitoka katika kituo rafiki kwa wanawake kwenye makazi ya wakimbizi wa Rohingya huko Cox's Bazar nchini Bangladesh. Kwenye kituo hiki angalau wana uhakika wa usalama wao.
UNFPA Bangladesh/Allison Joyce
Wanawake wawili wakitoka katika kituo rafiki kwa wanawake kwenye makazi ya wakimbizi wa Rohingya huko Cox's Bazar nchini Bangladesh. Kwenye kituo hiki angalau wana uhakika wa usalama wao.

Kwa mantiki hiyo amesihi Myanmar iwasilishwe ICC « ili madai ya uhalifu dhidi ya kibiinadamu na mauaji ya kimbari dhidi ya warohingya yaweze kuchunguzwa,na pia madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya makabila mengine kama vile Kachin na Shan nayo pia yachunguzwe. »

Kamishna Zeid pia ameomba Baraza hilo la Haki lipendekeze kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuanzishwa kwa jopo huru la kimataifa lisiloegemea upande wowote ambalo litakwenda Myanmar kusaidia uchunguzi wa vitendo vya uhalifu.

Amesema jopo hilo pia litawajibika kuandaa mfumo wa kujumuisha tena warohingya kwenye jamii zao na pia usaidizi kwa manusura wa janga hilo linaloendelea huko jimbo la Rakhine nchini Myanmar.
 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter