Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tafadhali subirini kabla ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Rohingya: UN

Warohingya wakivuka mto Naf ili kufikia kambi za wakimbizi nchini Bangladesh
© UNHCR / Andrew McConnell
Warohingya wakivuka mto Naf ili kufikia kambi za wakimbizi nchini Bangladesh

Tafadhali subirini kabla ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Rohingya: UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Mtaalam Maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa jili ya Myanmar ameisihi serikali ya Bangladesh kusimamisha mipango yake ya kuanza kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine mwezi huu, akisema kuwa serikali ya Myanmar imeshindwa kutoa hakikisho la ulinzi kwa wakimbizi hao.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis , Yanghee Lee, amesema hajaona ushahidi wowote wa serikali ya Myanmar ikichukua  hatua madhubuti  na bayana za kuweka mazingira bora  kuwezesha wakimbizi wa Rohingya ambao wako ukimbizini kuweza kurejea na kuishi kwa amani huku haki zao za kimsingi zikizingatiwa.

Serikali za Bangladesh na Myanmar, zilikubaliana Disemba 2017 kuhusu mpango wa kuwarejesha nyumbani kwa hiyari wakimbizi wa Rohingya walioko Bangladesh kuanzia katikati ya mwezi huu wa Novemba 2018.Lakini Lee amekuwa, akisema kila mara kuwa,  kurejea kokote kule kwa wakimbizi hao kabla ya kushughulikia chanzo cha mgogoro huo itakuwa ni kama kazi bure, na ametaka wakimbizi nao kuhusishwa katika mchakato huo kwani ni wao wenyewe walioamua kurejea makwao kwa hiari.

Hivyo mtaalam huyo amezihimiza serikali za Bangladesh na Myanmar kusimamisha mipango hiyo ya kuwarejesha nyumbani hadi pale ulinzi na usalama kwa wakimbizi wa Rohingya unaofuata  misingi ya sheria za kimataifa utakapohakikishwa.