Majadiliano ndio suluhu Afghanistan, kibarua ni kwa serikali na Taliban: Yamamoto

8 Machi 2018

Majadiliano ndio suluhu pekee ya kisiasa, kumaliza mgogoro, kuwaondolea madhila raia na kuleta amani ya kudumu nchini Afghanistan.

Kauli hiyo imetolewa leo na Tadamichi Yamamoto mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan wakati akihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, kuhusu hali na hatua iliyopiga nchi hiyo katika katika kuleta amani ya kudmu.

Amesema katika mkutano wa pili wa amani na usalama uliofanyika Afghnaistan wiki iliyopita washiriki wote waliidhinisha wito wa kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana baina ya serikali na waasi wa Taliban bila mashariti yoyote na kwamba

(TADAMICHI YAMAMOTO)

“Pande zote husika wakiwemo Taliban wanakubali kwamba majadiliano ya suluhu ya kisiasa ndio njia ya kukomesha machafuko, fursa ya majadiliano iko mezani sasa ni juu ya Taliban kuja na mapendekezo yao na kuanza majadiliano ya ana kwa ana na serikali ili kumaliza kwa watu wa Afghanistan.”

Ameongeza kuwa kuleta amani na kuwafuata wapinzani kwa muktada huo inahitaji moyo tena wa ujasiri, utashi wa kisiasa na zaidi ya yote umoja wa kitaifa.

Na kuhusu changamoto zingine hususani zinazowakabili wanawake hasa masuala ya haki, ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ushirikishwaji wao katika masuala ya amani na kuwawezesha kiuchumi na kisiasa amesema wanawake wa taifa hilo licha ya changamoto zote hizo wameonyesha mnepo na kutokata tamaa

(TADAMICHI YAMAMOTO)

“Mlishuhudia umuhimu wa haki za wanawake na kuwawezesha mlipozuru Kabul hivi karibuni na nina uhakika mliridhishwa kama mimi na mnepo walionao wanawake wa Afghanistan, uimara wao ndio unaoiunganisha jamii.”

Na kuhusu masuala tete ya uchaguzi amesema

(TADAMICHI YAMAMOTO)

“Tume huru ya uchaguzi IEC na mwenyekiti mpya wanajitahidi katika maandalizi lakini changamoto inasalia kuwa muda ni mdogo, mwenyekiti wa IEC alikiri kwamba uchaguzi huenda ukachelewa zaidi ya tarehe ya sasa ya Julai 2018 lakini bado unaweza kufanyika mwaka huu endapo maandalizi hayatocheleweshwa na uandikishaji wapiga kura ukianza Aprili kama ilivyopangwa.”

Amesisitiza pia kuwa ni muhimu kuwaelimisha raia wa Afghanistan kuelewa umuhimu wa kujiandikisha na kupiga kura japo wanamashaka na mfumo wa uchaguzi kwa sababu ya waliyoyapitia chaguzi zilizopita.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter