Idadi ya raia waliouawa na kujeruhiwa Afghanistan 2018 imefurutu ada:UNAMA

15 Julai 2018

Takwimu ziliotolewa leo na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, zinaonyesha kuendelea kwa idadi ya mauaji na kujeruhiwa kwa raia kunakochangiwa na pande zote katika mzozo nchini Afghanistan.

Katika kipindi cha kuanzia Januari Mosi hadi Juni 30 mwaka huu takwimu zinaonyesha raia zaidi ya 1692 wameuawa ikiwa ni idadi kubwa zaidi ikilinganishwa na wakati wowote ule katika miaka 10 iliyopita na raia wengine 3430 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa UNAMA idadi ya vifo imeongezeka kwa asilimia moja huku idadi ya majeruhi ikipungua kwa asilimia 5. Mpango huo unasema idadi ya raia wanaojeruhiwa na kuuawa bado iko juu licha ya kuwa na muafaka wa kusitisha uhasama kwa siku tatu baina ya serikali na kundi la Taliban mnamo Juni 15-17 mwaka huu 2018.

Mkuu wa UNAMA Tadamichi Yamamoto ambaye pia ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan amesema , “Usitishaji uhasama ulidhihirisha kuwa mapigano yanaweza kusitishwa na kwamba raia wa Afghanistan hawahitajitena kubeba gharama ya vita , tunaziomba pande zote kutumia furs azote zilizopo kusaka muafaka kwa njia ya amani, hii ndio njia bora zaidi ambayo watawalinda raia wote.  “

UNAMA inasema mashambulizi ya vikundi vitavyoipinga serikali kwa kutumia mabomu na vifaa vinavyolipuka bado yanashikilia usukati katika kusababisha vifo na majeruhi, ikiwemo mashambulizi ya kujitoa muhanga .

UNAMA imeorodhesha asilimia 52 ya majeruhia na vifo vya raia vimesababishwa na mashambulizi ya kujitoa muhanga na mengineyo ya mabomu kutoka kwa Daesh/ISKP hususan mjini Kabul na jimbo la Nangarhar.  Nalo kundi la Taliban liliwajibika na asilimia 40 huku aslimia iliyosalia inawahusu wapinzani wasiojulikana wa serikali. 

Nasafi ya pili imeshikiliwa na makabiliano ya ardhini ikifuatiwa na mauaji ya maksudi na ya kulengwa, operesheni za anga, na magruneti. Hofu kubwa ya UNAMA ni kwamba idadi ya vifo na majeruhi vinavyosababishwa na vikundi vinavyopinga serikali inaendelea kuwa juu kila uchao.
 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter