Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kufungua ukurasa mpya kwa Haiti- Mohammed

Ni wakati wa kufungua ukurasa mpya kwa Haiti- Mohammed

Sasa hivi gilasi ni nusu na ni wajibu wetu kuijaza, hiyo ni kwa mujibu wa naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J Mohammed akizungumza nchini Haiti wakati wa ziara yake nchini humo.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema licha ya kwamba kulikuwa na doa katika udhibiti wa mlipuko wa kipindupindu Haiti lakini Umoja wa Mataifa umechukua hatua ambazo zimezaa matunda na kufikia asilimia 99 ya kupungua kwa usambazaji wa kipindupindu na hivyo wananchi wa Haiti, wadau na Umoja wa Mataifa wote wamekuwa na mchango mkubwa katika kufikia hilo na ni muhimu wapongezwe.

Hatahivyo katika ziara yake aliotaja kama ishara ya kuonyesha mshikamano wa Umoja wa Mataifa na Haiti amesema ameshuhudia watoto na wanawake ambao wanaugua kipindupindu, huku akitiwa matumaini na wale ambao wanapata nafuu lakini akiongeza kwamba wanachotaka raia Haiti ni visa sufuri vya kipindupindu.

Bi. Mohammed amesema ametiwa moyo na juhudi za vijana ambao wamechukua hatua  kuelimisha jamii kuhusu usafi wa mazingira. Ameongeza kwamba alifanya ziara na msafara wa rais na katika nyuso za watu kulikuwa na masuali kuhusu msafara huo unaashiria nini

(Sauti ya Amina)

“Kile tulichoona ni maono ya miundo mbinu bora, msafara ulikuwa unasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kilimo na huduma za barabara, huduma ya kujisafi, maji na hii ni hatua ya kwanza. Na hatua hii ni muhimu kwa sababu inatoa mwelekeo wa njia ipi Haiti inapaswa kufuata.”

Kwa mantiki hiyo ametolea wito wadau kushirikiana na Haiti katika kujenga taasisi thabiti na kuwekeza katika Haiti ili kuwezesha nchi hiyo kufikia malengo ya maendeleo ya endelevu SDGs ifikapo 2030.